Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya kodi na faini ya jumla ya Sh
milioni 258.5 kutokana na bidhaa mbalimbali za magendo zilizokamatwa
katika kipindi cha Februari na Machi mwaka huu.
Hayo
yalisemwa jana na Mkurugenzi huduma na elimu kwa mlipa kodi Richard
Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema
bidhaa hizo zilikamatwa katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Kilimanjaro,
Mwanza, Kagera na Arusha katika operesheni inayoendeshwa kwa ushirikiano
kati ya TRA na Jeshi la polisi kudhibiti uingizaji wa bidhaa kwa njia
ya magendo nchini.
Aliongeza
kuwa katika Mkoa wa Kagera, TRA imekusanya sh milioni 120.4 kutokana na
kukamata katoni 2,043 za pombe aina ya Signature Vodka kutoka Uganda
ambazo ni sawa na lita 24,516 yenye thamani ya sh milioni 61.9
zilizokuwa katika Jahazi ya MV Tabasamu TMZ 0541.
Kodi
ya Sh milioni 66.7 ilipatikana baada ya madumu 1,599 ya lita 20 za
mafuta ya kupikia yenye thamani ya Sh milioni 65.9 kukamatwa Morogoro na
kulipa kodi pamoja na faini.
Pia
alisema katika Mkoa wa Tanga madumu 888 ya lita 20 za mafuta ya kupikia
yenye thamani ya Sh milioni 15.3 yalikamatwa eneo la Kwame katika
bandari bubu wilayani Mkinga.
Alisema
kwa kutumia taarifa kutoka kwa msamaria mwema jumla ya lita 2,290 za
mafuta ya taa yenye thamani ya sh milioni 2.7 yalikamatwa mkoani Arusha
yakiwa yamepakiwa katika gari aina ya Toyota Hiace yakisafirishwa kutoka
Holili kwenda Moshi kwa magendo.
Katika
hatua nyingine, TRA mkoani Mwanza ilikamata jahazi lijulikanalo kama MV
Kalebezo ikiwa na lita 50,000 za mafuta ya taa kutoka Kenya ambayo
yameingizwa nchini kinyume na taratibu za kisheria.
إرسال تعليق