Raha ya kipindi tunachoishi sasa ni wepesi wa mawasiliano.
Mawasiliano ya haraka kwa simu za mkononi, habari kusambaa, mitandao
kutupasha yaliyotokea, ghafla bin vuu. Hakuna linalofanyika hadharani
likapita, vuum, siku hizi. Iwe umbea au udaku; serikali, mazuri au
kashfa, gharika au tufani; ili mradi...Buum! Hiyo hapo machoni.
Hata mambo ya binafsi ambayo miaka 25 iliyopita
yaliwekwa uvunguni. Ya mtoto kuzaliwa, mtu kuonyesha chakula alichokila,
wanawake kutangaza madoido na urembo wao wa kucheza na kukata viuno,
nk. Tunaishi msimu wa majigambo ya nafsi. Kutaka kuonekana, kusifiwa
kujinadi hadharani; kwa uzuri au ubaya. Kila mtu ajue.
Kiingereza kina neno lake maalumu la kifalsafa.
“Narcissism”....lenye asili Uigiriki. Enzi
Wagiriki wakitawala maendeleo (kama Marekani leo) Narcissus, kijana wa
kiume aliyekuwa na haiba maridadi, alijienzi kiasi ambacho siku moja
Nemesis mwanamke wa kuvutia, akamghilibu ajitazame katika dimbwi la
maji. Narcissus alivyokuwa na huo upendo wa wajihi wake alikaa pale
akijifurahia alivyokuwa mrembo. Kumbe ule wasifu aliouona majini
ulikuwa picha tu. Njozi.
Sasa Narcissus akawa anapotelea ndani ya hiyo
njozi ya wajihi wake, akijifurahia hadi alipojisahau na kuanguka
dimbwini. Akafa. Ndiyo maana ipo nahau ya Kiingereza isemayo “he met his
nemesis” au “she met her nemesis”...yaani, mtu unakutana na Ibilisi au
jambo linalokuweza na kukuangamiza. Nemesis alimtega na kuchangia
kuaangamia kwa Narcissus si kwa ubaya ila kutokana na kujipenda kuzidi
kawaida.
Mantiki ya kisa inatufundisha nini kuhusu lugha, maisha na maudhui?
Tuko ndani ya mazingira ya kupenda umaarufu na
kujitangazia lolote tunalolifanya na kulishirikisha kwa yeyote yule.
Ndani ya mazingira yetu mna hulka ile ya methali ya Kiswahili, “ Hapana
siri ya watu wawili...”
Raha imo, ndiyo. Kufichua mabaya. Polisi weupe wa
Kimarekani sasa hivi wanakosolewa kutokana na vitendo vyao vya kuua
watu weusi waliovunja sheria mitaani bila kuwafikisha mahamakani. Siyo
kwamba ni mambo mapya. Tangu enzi magenge ya weupe yakiwavizia watu
weusi na kuwanyonga hadharani kwa kosa dogo la kutongoza msichana wa
Kizungu. Yalitendeka. Tofauti? Leo huwekwa hadharani kutokana na vifaa
kama simu za mkononi na video zilizozagaa barabarani majuu (CCTV).
Raha ya mablogu ndiyo hiyo.Ufidhuli na ufisadi wa
viongozi wapotofu unachojolewa soksi, sidiria na kofia. Kama ilivyotokea
vuguvugu za Mashariki ya Kati (Arab Spring): Tunisia, Libya, Misri na
kuishia viongozi waliowatesa wananchi kutolewa madarakani. Kifo katili
cha Kanali Muammar Gadaffi mwaka 2011 mathalan, kiliwekwa wazi.
Uanahabari wa kijamii kilingeni.
Hapa kwetu Tanzania mwanahabari wa TV, Daudi
Mwangosi alipouawa kinyama mwaka 2012, picha ya viungo vyake vya ndani
(utumbo na kadhalika) ziliwekwa wazi wazi mitandaoni. Sasa hivi
ukibofya tu Daudi Mwangosi, vimeselelea mitandaoni. Wanablogu
walikuwa watu wa kwanza kuonyesha ukatili wa askari walioyateketeza
maisha ya Mwangosi akiwa kazini na kuiacha familia yake ikilia mayowe
hadi mtondogoo.
Mabloga ni wanahabari huria
“Houria” ni uhuru kwa Kiarabu. Uhuria huu
uliochipuka mwaka 1990 baada ya kuanguka himaya ya Ukomunisti na
kubomolewa ukuta uliotenganisha Ujerumani ya Mashariki na Magharibi,
mjini Berlin. Mengi yaliyofuatia hapo yameweka utamaduni wetu sasa.
Kufunguliwa Nelson Mandela kutoka jela baada ya miaka 26. Akaanzisha
serikali mpya iliyo ahueni na kiini cha safari za Waafrika wengi
kushuka Afrika Kusini. Wagonjwa wetu kwenda kutibiwa, ushirikiano wa
kibiashara, runinga na vipindi vya TV, nk. Pia kuanzishwa kwa vyama
mbalimbali vya kisiasa barani Afrika. Uhuria huu ulituathiri pia katika
starehe; tuna muziki wa kizazi kipya ...muziki wa Bongo Fleva. Umejenga
ajira kwa vijana wanaojituma, kutegemea muziki. Kinyume na miaka 35
iliyopita siku hizi tunao wanamuziki matajiri kuliko enzi za marehemu
Patrick Balisidja, Mbaraka Mwinshehe, Kiko Kids na Marijani Rajab. Tuna
vyama vya upinzani na wanasiasa chipukizi mathalan Zitto Kabwe na
January Makamba. Enzi za Tanu kiongozi kijana alikuwa Chediel Mgonja
aliyeingia baraza la mawaziri akiwa na umri mdogo wa miaka 31-33.
Haikuwa kawaida na siyo wengi wanamjua Mgonja aliyekuwa Waziri wa Elimu
kadhalika. Alipofariki mwaka 2009, mmoja wa watoa maoni ndani ya blog
la Michuzi alisifia:
إرسال تعليق