Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kila mwanachama
anapaswa kuwaunga mkono wagombea watakaopitishwa na chama hicho katika
nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwani kinyume chake ni
kukisaliti na adhabu yake ni kufukuzwa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira alisema
mwishoni mwa juma kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi
Mkuu, chama hicho kinahitaji nguvu za pamoja.
“Sisi bado hatujajiunga na Ukawa, hivyo wanachama
wetu wanapaswa kulitambua hilo na kuepuka kushiriki kwenye ushawishi wa
kufanya kampeni za wagombea wa vyama vingine. Hata kwenye katiba yetu
tunasema sasa tunalenga zaidi katika kujiimarisha ili kutoa ushindani
mzuri wa kisiasa katika uchaguzi huu,” alisema.
Katiba ya ACT, imeeleza wazi kuwa pamoja na sababu
nyingine na kwa mujibu wa kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu,
mwanachama yeyote ambaye atasaidia kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la
kuunga mkono chama kingine au mgombea wakati chama kimeweka mgombea wake
kwa mujibu wa sheria za nchi, atakuwa amepoteza uanachama wake.
ACT- Wazalendo tayari imetoa ilani yake ya
uchaguzi ikionyesha kwamba iwapo itaingia madarakani, itawajibika kwa
wananchi kwa kuweka kipaumbele katika maeneo manne ambayo ni hifadhi ya
jamii, uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, afya na
elimu.
Kauli hiyo ya ACT linakuja huku kambi ya vyama
kadhaa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
ikiwa kwenye mchakato wa kuunganisha nguvu ili kusimamisha mgombea mmoja
wa urais na kuachiana majimbo katika baadhi ya maeneo.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia amewahi
kunukuliwa akisema kuwa umoja huo unaoundwa na Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD umehamishia nguvu zake kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mbatia alisema tayari umoja huo umeunda kamati
maalumu kutafuta namna ya kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na
kuachiana majimbo.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
alisema tayari kamati zimeundwa na zinaendelea na kazi ya kuratibu
mpango huo mahsusi, unaolenga kuiondoa CCM madarakani.
“Lengo letu ni kuhakikisha Ukawa ina nguvu ya
kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na katika mpango huo, vyama
vitaachiana majimbo na viti vya udiwani kulingana na nguvu ya chama
katika sehemu husika,” alisema.
Mkakati huo uliopangwa na Ukawa, unaelezwa na
wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni kombora kwa CCM, kwani endapo
utafanikiwa, utakiweka chama hicho tawala katika wakati mgumu katika
Uchaguzi Mkuu uliopangawa kufanyika Oktoba mwaka huu.
إرسال تعليق