GAZETI hili jana tulichapisha ripoti ya utafiti iliyokuwa ikieleza
kuwa Jeshi la Polisi nchini limeingia lawamani kutokana na kudaiwa kuwa
linahudumia zaidi watu wenye fedha kuliko wananchi wa kawaida.
Utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Twaweza unaonyesha kuwa wananchi
sita kati ya 10 sawa na asilimia 60 wanaamini jeshi hilo linawahudumia
zaidi watu wenye fedha kuliko Watanzania wa kipato cha chini.
Pia, kwa mujibu wa utafiti huo matukio ya ukatili dhidi ya polisi
yameongezeka, wananchi wawili kati ya 10 ambao ni asilimia 21 wamesikia
matukio ya aina hiyo na kwamba mwaka jana ni mwananchi mmoja kati ya 10
aliyeyasikia matukio kama hayo.
Utafiti huo unaonyesha kuwa kutokana kupungua kwa imani na jeshi la
polisi, watu wengi wameamua kuanzisha vikundi vya usalama vya kijamii
ambavyo husimamia utekelezaji wa sheria za kawaida ambako wanaripoti
matuko hayo.
Tunachukua nafasi hii kuipongeza Taasisi ya Utafiti ya Twaweza kwa
kufanya utafiti huu ambao umetoa picha ya hali ilivyo ndani ya jeshi la
polisi nchini.
Hii sio mara ya kwanza kwa tafiti mbalimbali zilizowahi kufanywa
kuinyoshea kidole jeshi la polisi kwamba linahusika na ukiukwaji wa haki
za binadamu au linajihusisha na vitendo vya rushwa.
Mwanzo nwa mwaka huu Taasisi ya Afrobarometer ilitoa ripoti
ya utafiti wake ukionyesha kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) ni kati ya taasisi zilizoshika nafasi za juu kwa kupokea
rushwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Utafiti huo ulilihusisha
jeshi la polisi katika vitendo hivyo.
Tunachukua nafasi hii kulitaka jeshi la polisi kutumia ripoti za tafiti hizi kujitathmini na kuchukua hatua za kujisafisha.
Tunaamini kuwa tafiti hizi zote zimefanywa kisayansi kwa kuwauliza wananchi ambao majibu ndiyo yamekuwa msingi wa ripoti hizi.
Jeshi la polisi kazi yake ni kulinda raia na mali zao, lakini
linapoanza kuhusishwa na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na
kupokea rushwa, ni hatari sana katika ustawi wa nchi.
Ni wazi kuwa wananachi watapoteza imani na jeshi hilo na matokeo yake
wananchi wanaweza kujiingiza katika vitendo vya kujichukulia sheria
mkononi.
Hivi sasa wananchi wanapomkamata mhalifu humkumu kwa kumchoma moto au
kumuua kwa kipigo wakiamini kuwa wakimpeleka polisi huenda akaachiwa.
Ni vyema sasa jeshi la Polisi lijisafishe kwa kuwaondoa kazini askari
ambao wanajihusisha na rushwa na vitendo vingine ambavyo vinalipaka
matope, ili wananchi waendelea kuliamini na kutoa ushirikiano wa
kudhibiti wahalifu.
- Jamboleo
Post a Comment