Indonesia yajitetea kwa kuwaua wanane

JAKARTA, Indonesia
INDONESIA imetetea uamuzi wake wenye utata wa kuamua kuwauwa wafanyabiashara wanane wa dawa za kulevya wakiwemo raia saba wa kigeni kwa kile ilichodai kuwa hivyo ni vita dhidi ya biashara ya mihadarati.
Kwa upande wake, Australia imemuita nyumbani balozi wake Nchini Indonesia kama hatua ya kulalamikia kuuawa kwa raia wake wawili waliohusika na biashara hiyo.
Waziri Mkuu, Tony Abbott, alisema ingawa anaheshimu utawala wa Indonesia kama taifa huru, uhusiano wa mataifa hayo mawili hautaendelea kama kawaida baada ya mauaji ya raia hao wawili.
Mkuu wa sheria nchini Indonesia, Muhammad Prasetyo, alisema hatua ya Ausralia kama hasira za muda mfupi tu.
Waustralia hao waliuwawa kwa kupigwa risasi na kikosi maalum cha wauaji pamoja na washukiwa wengine sita dawa za kulevya.
Licha ya vilio vya kuwasamehe watu hao kutoka kwa mataifa mbalimbali duniani, Indonesia iliamua kwa vyovyote kuwaua.
Kuuawa kwa mfungwa wa tisa, raia wa Ufilipino, Mary Jane Veloso, kumecheleweshwa na Rais Joko Widodo, baada ya mwanamke mmoja kujiwasilisha kwa polisi nchini Ufilipino, akisema kuwa ndiye aliyemhadaa mfungwa huyo mwanamke mwenzake, kupeleka dawa za kulevya Indonesia.
Brazil nayo imesema kuwa kuuawa kwa raia wa pili wa Brazil nchini Indonesia, katika kipindi cha miezi minne, ni hatua ya kukatisha tamaa na tayari imeyumbisha vibaya uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa hayo mawili.

Post a Comment

Previous Post Next Post