THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website : www.ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425 |
|
PRESIDENT’S
OFFICE,
STATE HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho amepokea kwa
majonzi na simanzi kubwa taarifa za kifo cha mmoja wa watumishi wa miaka mingi
wa Serikali, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), Chama cha TANU na
Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Africa – Liberation
Committee of the African National Unity (OAU), Brigedia Hashim Mbita,
kiongozi ambaye Rais Kikwete amemwelezea kama mmoja wa viongozi ambao
wameifanyia nchi yetu mengi na kwa miaka mingi.
Rais
Kikwete ambaye amepokea taarifa za msiba huo mara ulipotokea asubuhi ya leo,
Jumapili, Aprili 26, 2015 wakati alipoingia tu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam,
kuongoza maelfu kwa maelfu ya wananchi kuadhimisha miaka 51 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, ameuelezea msiba huo kama msiba wa simanzi kubwa.
“Ni wachache
katika nchi yetu wanaoweza kulinganishwa na Mzee Hashim Mbita kwa kiwango cha
utumishi uliotukuka, wa miaka mingi na usiokuwa na kasoro. Katika utumishi wa
Serikali alipata kuwa Mwandishi wa Habari Mkuu wa Idara ya Habari na pia kuwa
Mwandishi wa Habari wa Rais kabla na baadaye kuwa Balozi wa Tanzania katika
Zimbabwe. Kazi zote alizifanya kwa ufanisi mkubwa sana,”amesema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Katika
Chama cha TANU alikuwa Katibu Mtendaji wa Chama na katika Jeshi letu makini,
Mzee Mbita alipata na kufikia cheo cha Brigedia Jenerali, yote mambo makubwa
kweli kweli.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Lakini ilikuwa katika nafasi ya Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi
ya Umoja wa Afrika ambako Mzee Mbita alikamilisha utumishi wake kwa kusimamia
shughuli nzito ya kuwasaidia ndugu zetu Kusini mwa Afrika kwa miaka 20
mfululizo, miongo miwili, na kuweza kupata uhuru wao. Hakuna mpigania uhuru
katika Mozambique, katika Zimbabwe, katika Namibia, katika Angola na hatimaye
katika Afrika Kusini ukiondoa nchi nyingine kama Cape Verde, asiyejua mchango
wa Mzee Mbita. Wote hawa amewatumia vizuri, kwa ufanisi, kama mlezi, kama
kiongozi, kama kamanda hadi wakafanikisha kazi ya ukombozi. Huu ni mchango
mkubwa kweli kweli.”
Ameongeza
Rais: “Kitendo chake cha mwisho cha utumishi, kilikuwa kuongoza shughuli za Mradi
wa Hashim Mbita wa Kuweka Kumbukumbu za Harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika
na Kuenzi Viongozi Wakuu (Hashim Mbita
Project to Honour Outstanding Leaders), kazi ambayo nayo aliifanya kwa
uwezo na ufanisi mkubwa na ripoti yake tukaizindua mwaka jana pale Victoria
Falls, Zimbabwe wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).”
Ilikuwa
kwenye Mkutano huo wakati Zimbabwe ilitangaza kumpa Mzee Mbita Nishani ya The
Royal Order Munhumutapa yenye kutambua mchango wake katika harakati za
ukombozi wa Zimbabwe. Mzee Mbita amekuwa raia wa sita wa kigeni, na wa kwanza
asiyekuwa rais, kupata heshima hiyo ya juu kabisa ambayo hutolewa na Taifa la
Zimbabwe kwa wageni ambao wamechangia Uhuru wa Zimbabwe.
Viongozi
watano wa mwanzo kupata Nishani hiyo, mwaka 2005, walikuwa ni Marais na
Viongozi Waanzilishi wa Kundi la Nchi za Frontline States dhidi ya Ukoloni na Ubaguzi
wa Rangi, Marehemu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Kenneth David Kaunda wa
Zambia, Marehemu Sir Seretse Khama wa Botswana, Marehemu Samora Moises Machel
wa Mozambique na Marehemu Augustinho Neto wa Angola,
Ameongeza
Rais Kikwete: “Mzee Mbita ametibiwa ndani na nje ya nchi na kila alipolazwa hapa
nchini nilikwenda kumwona hospitali. Majuzi tu nilikwenda kumwona kwenye Hospitali
ya Jeshi letu pale Lugalo na tukazungumza vizuri sikujua itakuwa mara yangu ya
mwisho kuzungumza naye. Naungana na familia ya Mzee Mbita katika kuomboleza
kifo na msiba wa Mzee wetu huyu. Nawaomba watambue kuwa msiba wa Mzee Mbita ni
msiba wetu sote, msiba wa taifa letu ambalo limepoteza busara yake wakati
tulipokuwa tunahitaji zaidi.”
Ameongeza
Rais: “Tayari nimeagiza Serikali na Jeshi washirikiane na familia ya Mzee
Mbita katika kuandaa matanga na mazishi ya Mzee wetu huyu. Wakati tunaendelea
na maandalizi, nawaomba wanafamilia wawe na utulivu na subira kwa kadri
tunapopitia kipindi hiki kigumu na kwa pamoja tuendelee kumwomba Mwenyezi
Mungu, Mwingi wa Rehma kuiweka peponi roho ya Mzee Hashim Mbita. Amin.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
26 Aprili, 2015
Post a Comment