Mgogoro wa mipaka Tanapa wavuruga Mbunge, Wizara.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa.

Utekelezaji wa tafsiri ya mipaka kati ya makazi wilayani Mbarali na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), umekwama na kuibua mgogoro kati ya wananchi na viongozi wa serikali.
Hali hiyo ilibainika baada ya viongozi 19 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi za kata na wilaya kwenda Dodoma kumfuata Mbunge wao, Modestus Kilufi, ili wazungumze na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Walimtuhumu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa (pichani), kuwa yupo nyuma ya mgogoro huo akiwa na ajenda binafsi, ingawa Mgimwa alikanusha tuhuma hizo.
Ilielezwa kuwa akiwa na wakuu wa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya, mwezi uliyopita, Mgimwa aliwaeleza wakazi wa Mbarali kwamba kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (GN. 28) la Mwaka 2008 zaidi ya vijiji 21 vipo kwenye eneo la Tanapa, hivyo vinatakiwa kuhama.
Athanas Kikwembe, alisema kauli ya Mgimwa inapingana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete, kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 iliyotiliwa nguvu na GN. 28 lililotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu.
“Rais alisema GN 28 baada ya kuhamisha wenzetu wa Msangaji, hakuna hata mtu mmoja atakayehamishwa. Sasa Mgimwa anakuja na watu wake kusema zaidi ya vijiji 21 vihame kwa GN hiyo hiyo, hatutakubali,” alisema Makwembe.
Naye Mgimwa akizungumza na NIPASHE, alisema alikwenda Mbarali kutafsiri GN. 28 ili kila upande ufahamu kmipaka yake na kuiheshimu. Hata hivyo, kazi hiyo imekwama kwa alichoeleza kuwa ni kukosa ushirikiano wa wakazi hao na Kilufi. 
“Wakueleze kwanini mpaka leo GN. 28 haijatafsiriwa, mbunge anakimbia mikutano hata akipelekewa taarifa kwa maandishi, tuliishakutana na madiwani wote wanaohusika, lakini yeye akisikia anakusanya wananchi na kupeleka malalamiko kwa viongozi wakuu, akiwamo Waziri Mkuu,” alisema Mgimwa.
Alisema hakuna aliye juu ya sheria, GN 28 imetolewa kwa mujibu wa sheria, hivyo haina budi kutekelezwa na kuheshimiwa, ili itekelezwe lazima itatafsiriwe, jambo linalopingwa na Kilufi na wenzake na kuwa hakuwahi wala hatapingana na wakubwa wake.
Said Bahari Mwambarafu, alisema ingawa Serikali ina nguvu, mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na risasi za moto wamedhamiria kutetea haki ya kubaki kwenye makazi yao ya asili.
Kilufi alisema pamoja na wananchi kuteseka, CCM kisipochukua hatua za kumaliza tatizo hilo kijiandae kushindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Abdulkarim Warumba, alisema ingawa hawakukutana ana kwa ana na Kinana, walikutana na sekretarieti yake, ikawasikiliza kwa sababu zipo taratibu za vikao vya chama zilizokiukwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ya CCM.
Walitaka Kinana aishauri serikali ambayo inaongozwa na chama anachokiongoza itoe msimamo ikiwa wanahama au la kwa kuwa walichoahidiwa na Rais Kikwete ambacho kimo kwenye GN. 28 iliyohamisha wakazi wa Msangaji, kinatofautiana na kinachoelezwa na Mgimwa, inawakanganya.

Post a Comment

Previous Post Next Post