Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa.
Utekelezaji wa tafsiri ya mipaka kati ya makazi
wilayani Mbarali na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), umekwama na
kuibua mgogoro kati ya wananchi na viongozi wa serikali.
Hali hiyo ilibainika baada ya viongozi 19 wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ngazi za kata na wilaya kwenda Dodoma kumfuata Mbunge wao,
Modestus Kilufi, ili wazungumze na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana.
Walimtuhumu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa
(pichani), kuwa yupo nyuma ya mgogoro huo akiwa na ajenda binafsi,
ingawa Mgimwa alikanusha tuhuma hizo.
Ilielezwa kuwa akiwa na wakuu wa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya,
mwezi uliyopita, Mgimwa aliwaeleza wakazi wa Mbarali kwamba kwa mujibu
wa Tangazo la Serikali (GN. 28) la Mwaka 2008 zaidi ya vijiji 21 vipo
kwenye eneo la Tanapa, hivyo vinatakiwa kuhama.
Athanas Kikwembe, alisema kauli ya Mgimwa inapingana na kauli ya
Rais Jakaya Kikwete, kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010
iliyotiliwa nguvu na GN. 28 lililotolewa na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyarandu.
“Rais alisema GN 28 baada ya kuhamisha wenzetu wa Msangaji, hakuna
hata mtu mmoja atakayehamishwa. Sasa Mgimwa anakuja na watu wake kusema
zaidi ya vijiji 21 vihame kwa GN hiyo hiyo, hatutakubali,” alisema
Makwembe.
Naye Mgimwa akizungumza na NIPASHE, alisema alikwenda Mbarali
kutafsiri GN. 28 ili kila upande ufahamu kmipaka yake na kuiheshimu.
Hata hivyo, kazi hiyo imekwama kwa alichoeleza kuwa ni kukosa
ushirikiano wa wakazi hao na Kilufi.
“Wakueleze kwanini mpaka leo GN. 28 haijatafsiriwa, mbunge
anakimbia mikutano hata akipelekewa taarifa kwa maandishi,
tuliishakutana na madiwani wote wanaohusika, lakini yeye akisikia
anakusanya wananchi na kupeleka malalamiko kwa viongozi wakuu, akiwamo
Waziri Mkuu,” alisema Mgimwa.
Alisema hakuna aliye juu ya sheria, GN 28 imetolewa kwa mujibu wa
sheria, hivyo haina budi kutekelezwa na kuheshimiwa, ili itekelezwe
lazima itatafsiriwe, jambo linalopingwa na Kilufi na wenzake na kuwa
hakuwahi wala hatapingana na wakubwa wake.
Said Bahari Mwambarafu, alisema ingawa Serikali ina nguvu, mabomu
ya machozi, maji ya kuwasha na risasi za moto wamedhamiria kutetea haki
ya kubaki kwenye makazi yao ya asili.
Kilufi alisema pamoja na wananchi kuteseka, CCM kisipochukua hatua
za kumaliza tatizo hilo kijiandae kushindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Abdulkarim Warumba, alisema ingawa hawakukutana ana kwa ana na
Kinana, walikutana na sekretarieti yake, ikawasikiliza kwa sababu zipo
taratibu za vikao vya chama zilizokiukwa na uongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbarali ya CCM.
Walitaka Kinana aishauri serikali ambayo inaongozwa na chama
anachokiongoza itoe msimamo ikiwa wanahama au la kwa kuwa walichoahidiwa
na Rais Kikwete ambacho kimo kwenye GN. 28 iliyohamisha wakazi wa
Msangaji, kinatofautiana na kinachoelezwa na Mgimwa, inawakanganya.
إرسال تعليق