Mkasa huo wa kusikitisha ulioshuhudiwa live na mwanahabari wetu ulijiri kwenye nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Mindu Kata ya Uwanja wa Taifa mkoani hapa.
Awali, mmiliki wa nyumba hiyo iliyopo jirani na ofisi za Wakala wa Barabara Mkoa wa Morogoro (TANROADS), Mando Nahdi alimwamuru mwanamke huyo kuondoka kwenye nyumba yake lakini Jamila aligoma akidai hawezi kuhama hadi ajifungue.
Ilisemekana kwamba msimamo wa mwanamke huyo ulimkera mwarabu huyo ndipo akaita polisi ambao walifika na kumtimua msobemsobe huku akiwatolea maneno ya shombo akidai polisi walimchachafya.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mwanamke huyo alisema: “Nimekaa kwenye nyumba hii zaidi ya miaka mitano, sasa amenifukuza bila kunipa notisi, nilimwambia mume wangu hayupo asubiri nijifungue bado siku chache nashangaa ameniletea polisi.”
Mmiliki wa nyumba hiyo, alipohojiwa alisema: “Jamila hakupangisha bali alivamia na hajawahi kulipa kodi ya nyumba kwa muda wote alioishi.
“Mimi kama binadamu niliamua kumuacha lakini kwa sasa nahitaji nyumba yangu kwa matumizi anagoma kuondoka, nilikwenda ofisi ya kata kushtaki, viongozi wa kata pia aliwagomea kuhama wakaamua kuita polisi ambao wamemtimua kinguvu.”
Afisa mtendaji wa mtaa huo, Mwajuma Momboka alisema: “Kabla ya kuita polisi tulifika hapa na kusikiliza pande zote, kimsingi tumeona mwanamke huyu hakuwa mpangaji, alivamia nyumba ya watu na huruma ya mwenye nyumba alimuacha aishi kwa sasa mwenyewe anataka kuweka wafanyakazi wake.”
Wakati hekaheka hiyo ikitokea huku mwanamke huyo akitimkia kusikojulikana, mume wa Jamila aliyefahamika kwa jina moja la Banda alikuwa nje ya Morogoro kikazi.
Juhudi za mwandishi wetu za kumuombea mwanamke huyo kuishi hapo hadi mumewe atakaporejea ziligonga mwamba baada ya mmiliki wa nyumba hiyo kupatwa na hasira za mwanamke huyo kumtolea maneno ya kashfa.
إرسال تعليق