MTEJA: KISA NILIMKOPA CHIPSI, AKANILIPUA KWA MAFUTA YA MOTO!

Nusu kifo! Kijana aliyefahamika kwa jina la Hanafi Daudi (31), mkazi wa Salasala Kilimahewa jijini Dar, yupo katika hali tete kufuatia kumwagiwa mafuta ya moto yaliyokuwa yanakaangia chipsi.Hanafi ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Wodi ya Sewa Haji amesema aliyemchoma moto ni muuza chipsi ambaye alikwenda kumkopa chipsi.
Hanafi Daudi akiwa na majeraha usoni baada ya kuchomwa na mafuta ya moto.
Alisema tukio hilo lilijiri Machi 2, mwaka huu, Goba jijini Dar es Salaam ambapo yeye na wenzake wawili walikuwa wakilinda nyumba ambayo haijakamilika.
MSIKIE MWENYEWE
“Ilikuwa usiku wa saa 3:30 hivi, muda ambao watu walikuwa wanaangalia mpira. Ndipo nilipoamua kwenda pale  kwa lengo la kuomba kukopeshwa chipsi kwa kuwa sikuwa na pesa muda huo. Niliamini ningemlipa kesho yake.
Akiwa hospitali.
“Nilipofika, yule jamaa nilimuona kama yuko tofauti hivi lakini nikaamua nimuombe anisaidie kwa muda ule. Nikashangaa tu akanyanyua karai la mafuta ya chipsi na kunimwagia usoni.
“Nilihisi kuchanganyikiwa, nikakimbia mpaka kwa wenzangu. Wakati huo macho yote yalikuwa yameziba, sioni kitu chochote. Ndipo wenzangu wakanibeba na kunileta hapa Muhimbili kwa msaada wa usafiri njiani,” alisema Hanafi.
Akionyesha jeraha la mkononi
WENZAKE WAMKIMBIA
Akaendelea kusema: “Wale wenzangu baada ya kunifikisha hapa na kuondoka sijawaona tena mpaka leo. Sina msaada wowote, sina ndugu wa kunisaidia, sina mawasiliano na watu wa nyumbani Tanga.
“Najisikia vibaya sana kwa sababu mtuhumiwa alikimbia muda uleule aliponifanyia ukatili huu. Kikubwa ninamwomba Mungu anisaidie kwani yeye ndiye  anayejua cha kunifanyia.”
Moja ya jeraha alolipata mguuni.
ANAHITAJI MSAADA
Hanafi anaomba msaada kwa Watanzania waweze kumsaidia chochote kwa sababu mpaka sasa mwezi mmoja na zaidi umepita akiwa hospitalini hapo kwa kusaidiwa na manesi  kwa kuwa hana mtu wa kumuuguza.
“Ninaomba msaada angalau nipate pesa itakayonisaidia kununulia dawa kwa ajili ya kukaushia vidonda na nauli ya kuweza kunirudisha nyumbani kwetu, Tanga.”Kwa anayetaka kumsaidia, anaweza kutuma pesa kutumia namba 0712 121 330

Post a Comment

أحدث أقدم