NIKITA; MSANII WA KIKE ANAYECHEZA FILAMU ZA MAPIGANO BONGO

Hamida Hassan
Wengi wanamjua kwa jina la Nikita kutoka kwenye kiwanda cha filamu Bongo lakini jina lake halisi ni Elizabeth Chijumba, mwanamke aliyefanikiwa kufanya vizuri kwenye filamu mbalimbali zikiwemo za mapigano kama vile CID, We Are Four, Stolen Will, Well Done My Son na Adela.
Nikita ambaye ni mke wa msanii Khalfan Ahmad ‘Kelvin’ (mume wa zamani wa Yobnesh Yusuf ‘Batuli’) ni mwanamke pekee Bongo anayefanya vizuri kwenye filamu za mapigano.
Historia yake kwa kifupi
Alizaliwa mwaka 1982, elimu ya msingi akasoma Oysterbay Primary School ya jijini Dar kabla ya kuhamia Mzumbe Shule ya msingi iliyopo Morogoro.Baadaye alirudi tena jijini Dar katika shule ya msingi Kizuiani iliyopo Mbagala kufuatia  baba yake kuhamishiwa kikazi. Hapo akahitimu darasa la saba mwaka 1995.
1996 alianza Shule ya Sekondari Vosa Kongowe, akamaliza mwaka 1999 na safari yake kielimu ikaishia hapo.
Anusa umiss
Kwenye mambo ya urembo, Nikita anasema; “Mwaka 2000 nilijitosa kwenye Miss Kinondoni lakini kutokana na ufupi wangu niliambulia taji la Miss Kimara kisha safari ikaishia hapo.”
Ndoto za uigizaji zaanza
“Nilikuwa na ndoto za kuwa muigizaji hivyo niliamua kuwatafuta baadhi ya mastaa enzi hizo kama vile JB lakini sikufanikiwa kushaini.”
Ajiunga na chuo cha DSJ
“Mwaka 2003 nilijiunga chuo cha uandishi wa habari cha DSJ ambapo nilikutana na msanii wa Kundi la Sanaa Group aitwaye Dina ambaye siku moja aliniomba nimsindikize mazoezini, huko nikakutana na JB, akanipenda na kunipa kazi ya kwanza, nakumbuka ilikuwa ikiitwa Kanisa la Leo, hapo ukawa mwanzo wa mimi kuigiza.”
Magumu anayokutana nayo
“Kwa sasa nacheza sana filamu za action hivyo changamoto ni nyingi kwani nafanya na wanaume, natumia nguvu sana, kuna wakati naumia kweli lakini kwa sababu ni kazi ninayoipenda, naendelea kupambana.”
Mume anamchukuliaje
“Tukiwa kazini ni kazi, nikiumia ananihudumia kama wasanii wengine kwa sababu yeye ni dairekta, ila tukifika nyumbani anakuwa mume na mambo mengine yanaendelea kama kawaida.”
Mafunzo ya judo
“Sijawahi kupitia chuo cha judo ila mume wangu ambaye ndiye kiongozi wangu amekuwa akinifundisha sana staili hizo na sasa nimewiva kwa kiasi flani.”
Ashawishiwa na Cynthia Rothrock
“Msanii wa nje Cynthia Rothrock ndiye aliyenishawishi mpaka nikaamua kucheza filamu hizi kwani nilijiuliza kwamba, kama yeye ameweza na mimi nitashindwaje?”
Amzungumzia Batuli
Alipoulizwa kuhusiana na uhusiano wake na Batuli ambaye aliachwa na Kelvin kisha akaolewa yeye, Nikita alisema kuwa anamheshimu, kwanza kama msanii mwenzake na pia mzazi mwenzake na mumewe.
“Tukikutana tunaongea vizuri tu na mwanaye namlea kama wangu, namheshimu ananiheshimu,” alisema Nikita.
Atoa la moyoni
“Nawasihi mashabiki waangalie kazi za msanii siyo kuangalia kashfa. Mimi ninao uwezo wa kucheza filamu nyingi lakini waongoza filamu ‘madairekta’ ndiyo huwa wananipangia filamu za action na nazipenda kwa sababu nimezizoea.”

Post a Comment

أحدث أقدم