Rais Dkt.Jakaya Mrisho
Kikwete akimpongeza askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu
Liberatus Sangu wakati wa ibada ya kumweka wakfu iliyofanyika katika
kanisa kuu la Parokia ya Mama mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga
leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Aprili 12,
2015 ameungana na maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki, Jimbo la
Shinyanga, kuhudhuria Ibada rasmi ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu
mpya wa Jimbo hilo, Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu.
Rais Kikwete amewasili kwenye
Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma, Ngokolo, mjini Shinyanga kiasi cha saa
sita unusu mchana kwa ajili ya Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na
maaskofu wakuu, maaskofu na maaskofu wasaidizi 38, akiwamo Askofu Mkuu
wa Jimbo la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Rais wa
Mabaraza ya Kipapa na Katibu Mwambata wa Uenezaji Injili Ulimwenguni
Askofu Mkuu Protase Rugambwa kutoka Makao Makuu ya Kanisa Katoliki,
Vatican.
Askofu Sangu ambaye amewekwa
wakfu na kusimikwa kwenye Siku ya Huruma ya Mungu Duniani anakuwa
Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga na anachukua nafasi iliyoachwa wazi
tokea Novemba 6, 2012, wakati aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo, Baba
Askofu Aloysius
Balina alipofariki dunia. Kwa
miaka karibu mitatu, jimbo hilo limekuwa chini ya Usimamizi wa Kitume wa
Askofu Mkuu Yuda Tadei R’uaichii wa Jimbo Kuu la Mwanza.
Askofu Sangu mwenye umri wa
miaka 52 baada ya kuwa amezaliwa Februari 19, mwaka 1963, katika Kijiji
cha Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa, alipata daraja
la upadrisho Julai 3, mwaka 1994. Wakati anateuliwa na Baba Mtakatifu
Francesco kuwa Askofu Februari 2, mwaka huu wa 2015, alikuwa na daraja
la Mosinyori.
Akikabidhi Jimbo hilo kwa
Askofu mpya, Askofu Mkuu R’uaichii amesema kuwa Jimbo la Shinyanga ni
moja ya majimbo makubwa zaidi ya Kanisa Katoliki nchini, likiwa na
kilomita za mraba karibu 30,000 na waumini Wakatoliki wanaokaridiwa
kufikia 300,000 katika Mkoa ambao idadi kiasi ya wakazi wake bado
wanaamini imani za jadi.
Amesema kuwa Jimbo hilo lina
parokia 29, mapadre wa Jimbo 52, mapadre wa Kitawa 18 na hivyo kulifanya
jimbo hilo kuwa na jumla ya mapadre 70 na “jeshi kubwa” la watawa 70.
Kwenye sherehe hizo
zilizohudhuriwa na viongozi wengi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Mheshimiwa Ali Lufunga, Askofu Sangu amepewa zawadi ya sh
milioni 18, fimbo ya kiuchungaji na ng’ombe 10 wa maziwa na Wakatoliki
wa Jimbo hilo.
Rais Kikwete amerejea Dar es Salaam jioni ya leo baada ya kumalizika kwa Ibada hiyo.
![unnamed (13)](http://dewjiblog.com/wp-content/uploads/2015/04/unnamed-131.jpg)
Rais Dkt.Jakaya Mrisho
Kikwete akitoa salamu zake za pongezi muda mfupi baada ya kumalizika kwa
ibada ya kumweka wakfu askofu mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu
Liberatus Sangu katika Kanisa Kuu Parokia ya Mama Mwenye Huruma Ngokolo
Mjini Shinyanga.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj8EVZRFK8q6JPyIPfZNCA3wGDdN7iaeizA4m9ztfTz95moSAx2I-OKBzIO4g8eO88Z6hLACrcF5fJJlFRguBQEMQ7g-vYazpA_M2gWWKsRkKNHHVRNd-nNnES0Arl_kvoRM2kNUVDXrlhv/s1600/unnamed+(12).jpg)
Rais Dkt.Jakaya Mrisho
Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na maaskofu wa Katoliki muda mfupi
Baada ya ibada ya kumweka wakfu askofu mpya wa jimbo Katoliki Shinyanga
Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu(wapili kulia pembeni ya Rais) huko
Ngokolo mjini Shinyanga leo. (Picha na Freddy Maro)
Post a Comment