*Asema alianzisha ACT Wazalendo kwa sababu maalumu
*Asema kiongozi anayebeza Usalama wa Taifa ni wa ajabu
*Asema kiongozi anayebeza Usalama wa Taifa ni wa ajabu
Anicetus Mwesa
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ametoboa siri na kueleza alivyoshiriki kuanzisha chama hicho.
Pia, amesema ACT Wazalendo ni moto wa pumba hivyo Watanzania waache
kukidharau na badala yake waweke akiba maana katika siasa lolote
linawezekana, ikiwamo chama hicho kushika dola.
Alisema alifikia hatua hiyo baada ya kupokwa nafasi za uongozi ndani
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiwemo ya Naibu Katibu
Mkuu.
Zitto akizungumza katika mkutano wa viongozi wa ACT Wazalendo wakati
wa kujitambulisha kwa wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika Dar es
Salaam juzi, mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Kaskazini alikiri kuanzisha
Chama cha ACT Tanzania.
Akijibu swali aliloulizwa na mmoja wa wahariri, Zitto alisema hakuwa
na njia nyingine zaidi ya kuanzisha chama kwani aliona mizengwe ndani ya
Chadema dhidi yake haiishi.
“Hivi kweli wahariri mlifikiri ningekaa tu ilihali sitakiwi na baadhi
ya viongozi wenzangu ndani ya chama? Mimi nilishiriki kuanzisha chama
hiki kipya kwani sikuwa na njia nyingine zaidi ya kufanya hivyo.
“Hili nakuhakikishia nilishiriki, ila waraka unaoelezwa kwamba mimi
na wenzangu tuliuandaa hilo nakuapia kwa jina la Mungu na mama yangu
sikushiriki kuandaa waraka wowote ule, kwa mara ya kwanza niliuona
nilipoitwa kwenda kujieleza.
“Waraka uliandaliwa na Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na
wenyewe wapo hapa watasema ukweli wao. Kama nilivyowahi kusema sasa
hatuangalii nyuma tunaangalia mbele, muda wa kusema haupo,” alisema
Zitto.
Kuhusu kuhusishwa kwake na mawasiliano na watu wa usalama wa taifa,
Zitto alisema itakuwa jambo la ajabu kwa kiongozi wa chama cha siasa
kutowasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Jeshi la Wananchi au
Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.
“Basi utakuwa kiongozi wa ajabu sana kama hutakuwa na mawasiliano na
viongozi hao. Kuna wakati tulikuwa tunakaa kikao mimi na kiongozi
wenzangu wa chama pamoja na viongozi hao katika kujadiliana mambo
mbalimbali na wakati mwingine tunaitwa pamoja kupeana briefing au
anakwenda mwenzangu.
“Hili limetengenezwa na mwenzangu ambaye ametumia vyombo vya habari
kunichafua lakini ukweli anaujua ndiyo maana liliandika gazeti moja. Si
kwamba sikuwa na makosa mimi ni binadamu lazima kuna sehemu nilikuwa
nakosea,”alisema.
Pia, alisema chama hicho hakitaharibu mafanikio yaliyofikiwa na mfumo
wa vyama vingi hapa nchini na kwamba wanaheshimu vyama vyote vilivyopo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira alisema
chama hicho kipo tayari kushirikiana na chama chochote ambacho kipo
tayari kuboresha maisha ya Watanzania na kinachotaka kurejesha misingi
ya taifa.
Alisema chama hicho hakitachukua makapi ila wanawakaribisha wanasiasa wote ambao watakaokubaliana na Katiba ya ACT Wazalendo.
JLeo
إرسال تعليق