JK aahidi kushughulikia madai walimu kabla kustaafu.

Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete (pichani) ameahidi kuyashughulikia madai ya walimu kabla ya kuondoka madarakani.
Alitoa ahadi hiyo juzi jioni alipokuwa akizungumza na walimu zaidi ya 1,000 kutoka mikoa yote nchini.
Walimu walikutana katika Mkutano Mkuu wa Tano wa chama chao (CWT) unaoendelea.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliwataka kuacha mara moja kushiriki vitendo vya kuiibia serikali kwa kushirikiana kupiga ‘dili’ na wahasibu wa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi.
“Madeni mliyoyataja kwenye risala yenu tutaendelea na kazi ya kuyahakiki kwa kushirikiana na CWT na wakaguzi wa ndani,” alisema Rais Kikwete.
Aliwatahadharisha kuwa endapo ukaguzi ukifanywa utawakuta pia walimu na kushitakiwa kwa makosa ya kuiibia serikali.
Alitumia fursa hiyo kuwaaga walimu wote nchini, huku akisisitiza kuwa mambo, ambayo hakuyakamilisha, atayakabidhi kwa mrithi wake mara moja.
Katibu Mkuu wa CWT, Alhaj Yahya Msulwa, alimuomba Rais Kikwete kutekeleza mambo waliyomuomba kabla ya kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka huu, ikiwamo kutatuliwa uhaba wa walimu na posho za kufundishia.

Post a Comment

Previous Post Next Post