Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali haina nafasi
za ajira kwa sasa na kuwataka watu wasio na ajira kuelekeza nguvu zao
katika sekta binafsi.
Akihutubia sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi,
iliyofanyika kitaifa jijini Mwanza jana, Rais Kikwete alisema kwa sasa
serikali yake haina matumaini ya kuwapa ajira wale wasio na ajira bali
wanachotakiwa ni kutegemea zaidi sekta binafsi.
“Matumaini ya kupata ajira serikalini kwa sasa hakuna, bali kimbilieni katika sekta binafsi,” alisema Kikwete.
SEKTA BINAFSI
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema katika kipindi cha miaka 10 ya
uongozi wake kinachomalizika Oktoba, mwaka huu, serikali yake ilitoa
ajira zaidi ya milioni mbili, miongoni mwa hizo zaidi ya 600,000
zilitoka sekta za umma.
Alisema bado ukosefu wa ajira nchini ni tatizo kubwa na licha ya
utafiti mkubwa unaoendelea ili kuangalia soko la ajira, bado wananchi
wengi hawana ajira.
Alisema serikali yake ilifanikiwa kuboresha mishahara katika sekta
binafsi kutoka Sh.48,000 mwaka 2005 hadi kufikia 700,000 kwa baadhi ya
sekta binafsi.
“Wapo baadhi ya waajiri wanaolipa viwango visivyokubalika mpaka
sasa kwa wafanyakazi wao, ukiwauliza wanakupa visingizio vingi mara
uzalishaji umepungua,” alisema. Aidha, Rais Kikwete aliwapongeza
wakaguzi wa afya na usalama mahali pa kazi (Osha), kwa kufanikiwa
kufanya kaguzi 56,000 pamoja na kaguzi maalum 26,000 nchini.
Alisema kutokana na kazi zinazofanywa na Osha, serikali itaiimarisha ili iweze kufanya kazi kwa utendaji ulio bora zaidi.
WALIMU
Alisema muundo wa walimu umeidhinishwa na utekelezaji wake umeanza
Julai mwaka jana huku madai yao yakiwa zaidi ya Sh. Bilioni 53 kwa
serikali.
“Hawa walimu ambao ni shemeji zangu, wanatudai serikali zaidi ya
Sh. Bilioni 53 kwa ajili ya walimu 70,668 na tayari walimu 29,243
wamelipwa zaidi ya Sh. Bilioni 23,” alisema Rais.
Aidha, alisema madai ya walimu 30,807 ambao wanaidai serikali zaidi ya Sh. Bilioni 17, baada ya uhakiki uliofanywa majina
yalionekana yana kasoro, lakini malimbikizo ya walimu yanaendelea kufanywa na kulipwa kabla ya Agosti, mwaka huu.
Kadhalika alisema serikali inakusudia kuanzisha tume ya watumishi ya walimu ili waweze kuitumia pamoja na bodi itakayowahusu.
KODI
Kuhusu kodi, alisema serikali yake inaendelea kujitahidi kupunguza
kodi ya mapato kwa wafanyakazi kama ilivyofanya kutoka asilimia 18.5
mwaka 2007 hadi asilimia 12 sasa.
“Jambo hili tunafahamu linawaumiza zaidi wafanyakazi, lakini
tutajitahidi katika bajeti ya serikali ya mwaka huu kupunguza tena ili
iweze kukaribia asilimia 9…serikali ijayo nayo kama itaamua kupunguza,
itafanya hivyo,” alisema.
Aliwaagiza makatibu wakuu wa wizara zote kuhakikisha inawabana
waajiri ambao hawajaunda mabaraza ya wafanyakazi kwa kipindi kirefu.
Alisema mabaraza hayo yanatakiwa kukutana mara mbili kwa mwaka, na
wala kusiwe na kisingizio cha kutokuwa na pesa za kukutana, kwani mara
nyingi pesa za vikao wanakuwa nazo.
Hata hivyo, alisema kabla hajang’atuka kutoka katika uongozi
Oktoba, mwaka huu, atahakikisha anakutana na mabaraza hayo lakini pia
atamshawishi Rais ajaye kuendelea na utaratibu huo wa kukutana na
mabaraza ya wafanyakazi. Aliongeza kuwa changamoto za wafanyakazi nchini
haziwezi kumalizika kwani hata marais waliotangulia akiwamo Hayati Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa,
hawakuweza kumaliza kero za wafanyakazi nchini.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta),
Nicholas Mgaya, alisema changamoto wanazokumbana nazo wafanyakazi ni
pamoja na makato makubwa ya kodi ambayo wanataka yapunguzwe hadi kufikia
asilimia 9.
Mgaya alisema hali hiyo imekuwa ikiwaumiza wafanyakazi wengi hivyo
inachotakiwa serikali kuangalia upya katika bajeti ya 2015/16 iweze
kupunguza.
Aidha, Mgaya alisema waajiri wengi wamekuwa wakiwatisha wafanyakazi
bila kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria, hali inayochangia
kuzorotesha uchumi.
Alisema mawakala wa ajira nchini wamekuwa wakifanya mchezo kwa
waajiriwa kutokana na kugeuka waajiri badala ya kazi yao, hivyo lazima
waajiwa wapewe kipaumbele kazini.
Aidha, kuhusiana na ajali zilizotokea nchini katika miezi ya
karibuni, Mgaya alisema serikali ichukue hatua stahiki kuweza kudhibiti
ajali hizo za barabarani, kwani uwajibikaji ukiwepo lazima
zitadhibitiwa.
DK. SHEIN AAHIDI KULIPA MALIMBIKIZO
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia watumishi
wa umma kuwa serikali itawalipa malimbikizo ya madai yao yote mapema
mwaka wa fedha 2015/2016.
Akizungumza na wafanyakazi wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi Duniani jana yaliyofanyika katika viwanja vya Kiwanda cha
Mkonyo, wilaya ya Chakechake Pemba, Dk. Shein amewahakikishia watumishi
hao kuwa serikali inazifanyia kazi kasoro hizo na kuwahakikisha kuwa
hakuna mtumishi atakayepoteza haki yake.
Dk. Shein alibainisha kuwa hatua zote zinazochukuliwa na serikali
kuimarisha hali ya wafanyakazi, lengo lake ni kulifanya suala la
kuwapatia maslahi bora watumishi wa umma liwe endelevu kadri uchumi
unavyoimarika.
Miongoni mwa hatua hizo ni kupitisha sheria mbalimbali zikiwamo Sheria Na. 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011.
Dk. Shein aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa Serikali ipo katika hatua
za mwisho za kukamilisha Sera ya usalama kazini ili kuweka mfumo mzuri
wa afya katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwakinga wafanyakazi na
ajali na majanga mengine katika sehemu za kazi.
إرسال تعليق