Lipumba: Rais bora hawezi kutoka CCM

Tabora. Siku kadhaa tangu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kuwatahadharisha wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), ya chama hicho kwamba wanapaswa kumteua mgombea wa urais anayekubalika ndani na nje ya chama hicho, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kauli hiyo haina ukweli.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (pichani) amesema hakuna mtu anayefaa kuwa Rais ndani ya CCM, kwa kuwa mfumo wa chama hicho hauruhusu uadilifu.
Profesa Lipumba alisema hayo jana alipokuwa akihutubia wakazi wa Kijiji cha Kayombo wilayani Nzega.
Alisema  ndani ya CCM, kuna tatizo la kimfumo ambalo hata akitokea mtu mwadilifu akawa rais, bado atavurugwa na mfumo uliopo na kuwa fisadi.
“CCM kimekosa mfumo wa uadilifu hivyo hakiwezi kutuletea kiongozi wa nchi, kwani hata akitokea mtu mwadilifu akashinda, bado atavurugwa na mfumo huo wa kifisadi,” alisema Profesa Lipumba.
Sifa za Rais
Profesa Lipumba ambaye yuko mkoani Tabora kwa ziara ya kuhamasisha wananchi wajiandikishe kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, alisema kwa hali ilivyo, Tanzania inahitaji Rais mwadilifu ambaye kimsingi, hawezi kutokea CCM.
Alisema uongozi wa CCM hauthamini dira ya Taifa na tatizo hilo ndilo linalofanya wananchi wawe na maisha magumu kwa kukosa uhakika wa matibabu, elimu bora na chakula.
Profesa Lipumba alisema wananchi hawapati matibabu ya uhakika kwa kuwa zahanati na hospitali hazina dawa. Lakini hayo yakiendelea, viongozi wanakwenda kutibiwa nje ya nchi.
“Elimu nayo inatolewa kwa ubaguzi. Watoto wa maskini wanasoma sekondari za kata ambazo hazina walimu wala vitabu na watoto wa matajiri wanasoma shule zenye walimu na vitabu,” alisema.
Profesa Lipumba alibainisha kwamba endapo CUF itaingia madarakani, wananchi watapata haki mbalimbali zikiwamo za elimu, afya na haki nyingine tofauti na ilivyo sasa.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa uchaguzi ndiyo fursa ya kuitoa CCM madarakani na kwamba hawawezi kupiga kura kama hawajajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura

Post a Comment

Previous Post Next Post