MPENZI WA FACEBOOK AMNYONGA MKE WA MTU GESTI!

KWELI mchepuko siyo dili! Kauli hii imedhihirika kufuatia mwanadada, Ashura Maulid, mkazi wa Ilala jijini Dar, kukumbwa na mauti kwa madai ya kunyongwa ndani ya gesti na mwanaume mmoja anayejulikana kwa jina la Charles ambaye inasemekana ni mpenzi waliyekutana kwenye mtandao wa kijamaii wa Facebook.
Marehemu Ashura Maulid enzi za uhai wake.
Tukio hilo lililojaa majonzi tele na kuacha maswali mengi, hasa kwa mume wa marehemu, Suleiman Othman, lilijiri  Mei 19, mwaka huu kwenye nyumba ya kulala wageni (jina lipo) iliyopo kandokando ya barabara ya kutoka Sinza Afrikasana kwenda Kijitonyama kupitia Kituo cha Polisi cha ‘Mabatini’, Dar.
Chanzo kinadai kuwa, enzi za uhai wake, mwanadada huyo alikuwa akijihusisha na biashara ya kuuza duka la friji maeneo ya Sinza ya Afrikasana na inasemekana amekuwa ndani ya ndoa na mumewe, Suleiman kwa miaka 15 na kujaliwa kupata watoto wawili, wa mwisho akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.
Akizungumza na Uwazi, Ijumaa iliyopita huku akiwa katika majonzi mazito, mume huyo alisema Jumanne ya Mei 19, mwaka huu, mkewe alimuaga anakwenda kazini huku akiumwa, alimtaka apumzike lakini mwanamke huyo akasema anajiona amepona hivyo ana uwezo wa kumudu majukumu yake.
“Ilipofika saa moja usiku akanitaarifu kuwa ameshatoka kazini. Cha ajabu mpaka saa nne usiku alikuwa hajafika nyumbani na nilipompigia simu hakupokea.“Mara kwa mara mke wangu alipokuwa akimaliza kazi na kuanza safari ya kurudi nyumbani alikuwa ananitaarifu, nachati naye kila wakati mpaka anafika. Siku hiyo nilikuwa nina majukumu mengi aliponitaarifu kamaliza kazi ndo’ anarudi sikuwa na presha.
“Sasa ilipofika saa nne mimi nikiwa nyumbani na simu hapokei, nikashangaa. Mbaya zaidi, baadaye simu yake ikawa haipatikani kabisa.“Nilifanya jitihada za kumtafuta kwa ndugu na jamaa, vituo vya polisi na hospitali mbalimbali, ikiwemo Muhimbili kuulizia kwenye wodi za wagonjwa lakini sikumkuta.
Mume wa marehemu Ashura Maulid.
“Juzi (Mei 20), nilishtuka kupigiwa simu na polisi wa Kijitonyama, wakaniambia kuna maiti imekutwa mahali (walimficha kama ilikuwa gesti) na aliyehusika na mauaji ni mwanaume ambaye walianza kufahamiana na mke wangu kupitia Facebook. Walisema marehemu alionekana alikufa kwa kunyongwa.
“Waliniambia huyo mwanaume alikimbia baada ya kufanya mauaji hayo. Palepale ndo’ wakaanza jitihada za kumtafuta mpaka wakamkamata,” alisema mume huyo.Akiendelea kuelezea tukio hilo alisema kisa cha kugundua kuwa Charles alikutana na mke wake kwenye Facebook ni siku ya tukio baada ya mawasiliano waliyoyafanya kwa kipindi kirefu bila yeye kujua.
Alisema ilionesha kuwa, siku hiyo waliamua kuonana laivu ambapo alimkaribisha dukani kwake na kuondoka naye baada ya kumaliza kazi na kufunga duka huku akiwa amemtaarifu bosi wake (si mumewe) fedha zilizopatikana siku hiyo.
“Niliambiwa na rafiki wa mke wangu kuwa siku hiyo mwanaume huyo alifika dukani kwa mke wangu akawatambulisha mashosti zake kuwa ni rafiki yake waliyejuana Facebook. Wakiwa hapo, mke wangu  alimpigia simu bosi wake kumwambia siku hiyo aliingiza shilingi milioni moja na laki saba. Huenda hicho ndo’ kilimfanya jamaa amgeuke na kumuua kwa tamaa ya zile fedha,” aliongeza.
Mumewe huyo alisema, haamini kama mkewe alishindwa kuiheshimu ndoa yake na kuwapa nafasi wanaume wengine tena kwa kwa mtu ambaye hakufahamiana naye ila kwa kukutana naye kwenye mtandao na kuanzisha uhusiano kwani yeye alimtosheleza kwa kila jambo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura alipotafutwa ili aulizwe kuhusiana na tukio hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.Uwazi lilipofika kwenye gesti hiyo ambayo marehemu alifia chumba Namba 4 lakini wahusika  waligoma kutoa ushirikiano na kudai hakukuwa na tukio hilo.
Kesi  hiyo ipo katika Kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’ faili Namba KJN/RB/5081/15 TAARIFA YA KIFO huku mtuhumiwa akishikiliwa hapo baada ya kukamatwa akiwa na gari aina ya Toyota Carina (namba za usajili zipo).

Post a Comment

Previous Post Next Post