Zitto Kabwe Apinga Wabunge Kuongezewa Siku 10


KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kitendo cha Rais Jakaya kikwete, kuongeza muda wa bunge kwa siku 10 kwa ajili ya miswada 10 inalenga kupitisha miswada isiyojadiliwa kwa kina.

Amesema uamuzi huo utaiathiri nchi kwa kuwa wakati huu wabunge wengi wameelekeza akili zao katika majimbo wanayoongoza, hivyo hawatakuwa na muda mzuri wa kujadili kwa kina miswada hiyo kwa maslahi ya Taifa

Zitto alitoa kauli hiyo juzi mjini Kigoma wakati alipofanya mikutano miwili ya hadhara katika kata ya Nguruka Jimbo la Kigoma Kusini na baadaye Kigoma Mjini katika uwanja wa Centre.

Alisema kwa sasa wabunge wana wasi wasi na majimbo yao hivyo kutaka wajadili na kupitisha  muswada wa sheria ya mafuta na sheria ya matumizi yafedha za mafuta haiwezi kupewa umuhimu na wabunge hao

Badala yake Zitto aliitaka serikali isitishe miswada hiyo mpaka Bunge lijalo wakati wabunge watakapokuwa wametulia "ACT tunasema miswada hii isubiri Bunge jipya kwani ni miswada muhimu kwa nchi yetu, miswada inayohusu rasilimali za nchi haiwezi kukimbizwa haraka haraka  bungeni."

Alisema wasi wasi wa wabunge kwa wakati huu utachangia muswada huo kukosa umakini Alisema gesi na mafuta yamekaa ndani ya ardhi kwa muda mrefu na kwamba uharaka wa kujadili miswada hiyo haupo.

Alikumbusha kuwa Azimio la Tabora lililohuisha Azimio la Arusha linasema wazi sekta ya madini, mafuta na gesi ni muhimu na zinaweza kuzalisha mapato ya kutosha ya Serikali ili kuboresha sekta zingine kama kilimo na uwekezaji katika afya.

"Tunaitaka Serikali kuchochea mabadiliko  makubwa katika sekta hizi za uvunaji wa maliasili ya nchi kwa kuchukua hatua. "Maliasili zote za madini, mafuta na gesi ni mali ya wananchi kikatiba na uchimbaji wake lazima uwe na kibali cha wananchi, mikataba yote iwe wazi kwa wananchi," alisema Zitto.

Alisema Bunge lilitakiwa kumalizika Juni 27 mwaka huu kabla ya  Rais Jakaya Kikwete kuliongezea siku kumi zaidi kwa ajili ya kujadili miswada hiyo.

Akiwa katika Kata ya Nguruka Zitto alitumia muda huo kuwatahadharisha watu wanaotaka kugombea nafasi hiyo nje ya Chama cha ACT-Wazalendo kuwa wajitafakari mara mbili kama wataweza kupata ridhaa hiyo kwa wananchi.

Aliwaambia wakazi wa Kata ya Nguruka kama kuna watu wanaona wanakidhi kuwa wabunge wao watumie jukwaa la ACT-wazalendo vinginevyo wasiwape nafasi hizo. Aliwatahadharisha wananchi juu ya watu wanaowafikia na kuwaeleza kuwa watapambana na ufisadi pasipo kuwa na misingi ya kusimamia utekelezaji huo

"Sisi ACT-Wazalendo tukisema tunapambana na rushwa tunamaanisha kwa kuwa tumeweka jambo hili mpaka katika katiba yetu na kisha tukaliweka katika azimio kwa ajili ya utekelezaji," alisema Zitto.

Awali, wananchi waliohudhuria mkutano huo waliupokea msafara wa kiongozi huyo kilomita tano kabla ya kufika Kigoma mjini huku wengi wao wakiwa wanatembea kwa miguu na wengine wakiwa katika vipande mbalimbali.

Vijana wa mjini Kigoma walimlazimisha Zitto kushuka katika gari la wazi katika eneo la Gungu na kumtaka atembee kwa miguu kwa ajili ya kutoa fursa kwa watu kumsalimia.

Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika misafara hiyo kuanzia mapokezi hadi kufika uwanjani katika eneo la uwanja baadhi ya watoto walipotezana na wazazi wao kutokana na umati mkubwa wa wananchi walioshiriki mapokezi ya viongozi wa Chama hicho

No comments:

Post a Comment