
Anapokosekana kiungo wao, Salum Telela hali
inakuwa mbaya kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara. Mbuyu Twite
anayechezeshwa katika nafasi ya kiungo mkabaji ameshindwa kuimudu nafasi
hiyo vizuri.
Ukiacha Yanga ambayo ina safu laini kidogo ya
kiungo, kuna timu kadhaa za Ligi Kuu ambazo safu zao za kiungo ni
hatari. Zimejaa vijana mahiri ambao kazi zao hazina mashaka kabisa.
Makala haya yanakuletea orodha ya timu za Ligi Kuu
ambazo kama utakutana nazo ni vyema ukapandisha mashambulizi kupitia
pembeni maana katikati ni pagumu kupitika pengine kuliko safu nyingine
zozote za timu hizo.
Azam
Matajiri wa Bara, Azam wanaweza kuwa timu yenye
safu ngumu zaidi ya kiungo. Timu hiyo ina viungo sita tofauti ambao
wakicheza dimba la kati, basi shughuli yake inakuwa pevu.
Timu hiyo ina Frank Domayo, Himid Mao, Kipre
Bolou, Mudathir Yahya, Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ na Salum Abubakar
‘Sure Boy’. Mbali na hao pia Azam ina mkongwe Erasto Nyoni ambaye pia
anamudu kucheza nafasi ya kiungo.
Viungo hao wote wa Azam ni wa viwango vya juu,
wote ni wazuri katika kukaba na kupandisha timu. Kocha Stewart Hall
amekuwa akiwatumia viungo watatu kwa pamoja jambo ambalo linazipa shida
timu pinzani.
Mwadui
Hii ni timu mpya Ligi Kuu lakini usajili
iliyofanya unaonekana kabisa kuipa timu hiyo kiburi katika safu yake ya
kiungo. Mwadui ina viungo watano mahiri wenye uzoefu na Ligi Kuu huku
pia ikiwa na viungo wengine chipukizi. Safu ya kiungo ya Mwadui inaundwa
na mkongwe, Athuman Iddi ‘Chuji’, Jabir Aziz ‘Stima’, Anthony Matogolo,
Nizar Khalfan na Jamal Mnyate.
Uwepo wa Chuji, Stima na Matogolo kwa pamoja
katika timu hiyo ni ishara kuwa timu pinzani zijiandae kupita pembeni.
Viungo hao wote watatu ni wazuri katika kukaba, wanapiga pasi makini na
za uhakika. Ni vigumu sana kutawala dimba la kati mbele ya watatu hao.
Simba
Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, Simba wamemrejesha kundini
kiungo wao wa zamani, Mwinyi Kazimoto. Uwepo wa Kazimoto katika kikosi
cha Simba ni ishara kuwa timu hiyo itakuwa na safu ngumu pia ya kiungo.
Mbali na Kazimoto Simba ina Jonas Mkude, Abdi
Banda na Said Ndemla ambao ni mahiri pia katika dimba la kati. Mkude na
Banda ni wazuri katika kukaba na wanapandisha timu kama ilivyo kwa
Kazimoto.
Ndemla licha ya kuchezeshwa kama kiungo
mchezeshaji pia ni mzuri katika kukaba. Timu hiyo pia ina Peter
Mwalyanzi ambaye anamudu pia kucheza nafasi ya kiungo hivyo kuifanya
safu yao iwe imara zaidi.
Mtibwa Sugar
Pia ni mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, walikuwa na
safu imara zaidi ya kiungo msimu uliopita. Msimu huo Mtibwa ilikuwa na
Mussa Nampaka, Henry Joseph, Jamal Mnyate, Ibrahim Jeba, Mohammed
Ibrahim na Mkongwe Shaban Nditi ambao wote walionyesha kiwango cha juu.
Msimu huu ni Mnyate pekee aliyepungua katika safu
hiyo jambo ambalo haliachi pengo lolote. Nditi anaendelea kuwa nguzo
katika timu hiyo licha ya umri wake kusonga na amekuwa akiwapa tabu
viungo wa timu pinzani.
Uwepo wa Henry Joseph pia unaipa uimara zaidi
Mtibwa kutokana na soka lake maridadi, uwezo wake wa kukaba na kupiga
pasi za uhakika japo si kama alivyokuwa miaka mitatu iliyopita.
Mbeya City
Timu hii inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la
Mbeya haitishi tena kama ilivyokuwa katika msimu wake wa kwanza lakini
bado inaendelea kuwa na safu imara ya kiungo. Katika kipindi cha miaka
miwili timu hiyo imeondokewa na nyota zaidi ya 10 lakini haijaathirika
sana katika eneo la kati.
Usajili mpya wa Joseph Mahundi kutoka Coastal
Union na uwepo wa viungo wengine klabuni hapo kama Ken Ally, Raphael
Alfa na Steven Mazanda unaifanya timu hiyo iendelee kuwa na safu imara
ya kiungo.
Ni dhahiri kuwa timu zitakazokutana na Mbeya City zijiandae kupenya kupitia pembeni.
- Mwanaspot
Post a Comment