Ripoti za hospitali nchini na Shirika la Afya
Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa baadhi ya wanawake hutoa mimba kwa njia
zisizo salama, ambazo huharibu kizazi, kuwasababishia ugumba na wengine
vifo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika zahanati
na hospitali kubwa za wilaya jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa
asilimia kubwa ya wanawake hutoa mimba mitaani kwa kutumia njia za
kienyeji na wataalamu wasio na ujuzi. Baadhi ya njia zisizo salama
ambazo hutumika ni spoku za baiskeli, utomvu wa mti wa muhogo, vyuma
vyenye ncha kali na vidonge bila kufuata maelekezo ya madaktari.
Utomvu
huo una sumu ya ‘oxytocin’ inayoweza kuharibu mimba na wengine hutumia
vidonge vya “misoprostol” na “morning after” vyenye uwezo wa kuharibu
mimba, ambavyo vinauzwa kiholela katika maduka mengi ya dawa.
Hospitali ya Temeke
Kuanzia
Januari hadi Juni mwaka huu, zaidi ya wanawake 200 walifikishwa katika
hospitali hiyo wakiwa na matatizo ya uzazi, huku 12 kati yao
wakithibitika kujaribu kutoa mimba kienyeji.
Muuguzi
Kiongozi wa Wodi ya Sita katika hospitali hiyo, Mwasi Mwasamaga alisema
wanawake wengi wanaofikishwa hospitalini kutokana na kutoa mimba
kiholela huwa katika hali mbaya.
“Pamoja na kuwa
wanakuwa katika hali mbaya, mara nyingi hawasemi ukweli njia gani
waliyotumia kutoa mimba, lakini sisi kwa utaalamu wetu huwa tunajua kuwa
wametoa mimba,” alisema.
Muuguzi Kiongozi, katika
Jengo la Wazazi, Beatrice Temba alisema wanaofikishwa hospitalini hapo,
wengine huwa wamepata maambukizi kwenye kizazi, maambukizi hayo huweza
kuingia hadi katika mfumo wa damu na katika ogani zilizo karibu na
kizazi. Alisema wanawake wanaotoa mimba kiholela huwa wanatolewa na watu
wasiokuwa na ujuzi, wakati mwingine hupata madhara yanayosababisha
kizazi kutolewa kabisa, kupungukiwa damu kwa kiasi kikubwa, maambukizi
kwenye njia ya mkojo au kinga ya mwili kushuka na baadhi kufa.
Utafiti
wa Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili wa mwaka 2012 kuhusu utoaji wa
mimba uliofanywa katika kata za Wilaya ya Temeke umeonyesha kuwa
asilimia 33 ya wasichana walipata mimba zisizotarajiwa. Kati yao,
asilimia 26 walikiri kuzitoa na asilimia 87 zilitolewa kwa njia zisizo
salama ikiwemo kutumia spoku za baiskeli, miti ya muhogo, vitu vyenye
ncha kali na vidonge.
Katika utafiti huo uliofanywa na
Dk Neemba Mamboleo, wasichana 454 wenye umri wa kati ya miaka 19-25
walihojiwa na kukiri kuwa walitoa mimba kwa msaada wa marafiki wa kiume,
ndugu au wahudumu wa afya.
Kuhusu hilo, Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema utoaji wa
mimba ni kosa la jinai lakini pia aliuhusisha na uzembe.
Sophia
alisema elimu inatolewa kila mara kuhusu uzazi wa mpango huku njia za
kuzuia mimba zikitolewa bure kwa watu wa rika zote hata kwa wanafunzi
lakini watu hawazingatii.
“Chanzo kikubwa ni kuzikimbia
njia za uzazi wa mpango, hawataki kutumia hizi njia kuna kondomu,
vidonge, vijiti ambavyo maeneo mengine unavipata bure,” alisema.
Muhimbili
Takwimu
zilizopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinaonyesha kwamba mwaka
2010-11, walipatikana wagonjwa 35 walioharibika mji wa mimba kutokana na
utoaji mimba.
Kadhalika, takwimu za Muhimbili
zinaonyesha kuwa kati ya vifo 155 vya uzazi, 53 vilitokana na utoaji wa
mimba. Kitaifa mimba 2,430,000 zilitolewa kiholela na asilimia 18
zilisababisha vifo.
Mwananyamala/ Amana
Katika
Hospitali ya Mwananyamala, takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia Januari
hadi Juni mwaka huu wanawake 276 walifikishwa kutokana na kesi za
utokaji mimba. Kwa upande wa Hospitali ya Amana, wanawake 168
walifikishwa kwa matatizo ya utoaji mimba na kati yao, 18 wazitoa kwa
njia za kienyeji na walikuwa na maambukizi katika mfumo wa damu, kuoza
kwa kizazi au kutoboka.
Kwa mujibu wa madaktari,
wakunga na wauguzi katika hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana,
zaidi ya nusu ya wanawake wanaofika hospitali wakidai mimba zimeharibika
chanzo huwa ni wao kwamba wamezitoa kwa njia zisizo salama.
Muuguzi
Mkunga wa wodi ya wazazi wa Hospitali ya Amana, Eva Manyinye alisema
baada ya wanawake wengi kuhojiwa ili waweze kusaidiwa kwa urahisi hukiri
kutoa mimba kwa kutumia vifaa, kunywa dawa aina ya misoprostol na
wengine kwa kipande cha mti wa muhogo.
“Wakati mwingine wanakuja wanafunzi, tena wenye umri mdogo, wengine wanakuwa wameshaharibu kizazi kabisa,” alisema.
Waharibu vizazi
Uchunguzi
umeonyesha pia kwamba idadi kubwa ya wanawake wanaotoa mimba kiholela
aghalabu hutoboka utumbo, huchana kizazi, kizazi kuoza na wengine
kuharibu figo. Daktari wa Magonjwa ya Wanawake wa Hospitali ya CCBRT,
Fatma Suleiman alizungumzia madhara ya utoaji mimba na kusema ni bora
mwanamke anayetoa mimba asisubiri hali yake kuwa mbaya, bali afike
hospitalini mapema ili apewe matibabu.
“Kwa kawaida
sisi madaktari kazi yetu ni kuokoa maisha, hata kama amefanya kosa
lakini akifika hapa lazima atibiwe. Kwa hiyo, waje watibiwe na waseme
ukweli ni njia gani wametumia kutoa mimba, ili watibiwe,” alisema
Dk
Fatma alisema wanawake wengi siku hizi hutumia vidonge ambavyo huuzwa
kiholela kwenye maduka ya dawa, lakini huvitumia vibaya kwa kuzidisha
dozi au kutumia dozi ndogo hivyo kuwasababishia madhara makubwa, ikiwamo
kuchanika kwa kizazi au kupoteza maisha.
“Wengi
tuliowahudumia wanachanika kizazi au kile kidonge kinaua kiumbe, kiumbe
kinashindwa kutoka mpaka kizazi kinaoza,” alisema.
Hatari ya ‘misoprostol’
“Hivi
vidonge vya ‘misoprostol’ awali vilikuwa vinatumika kutibu vidonda vya
tumbo na kuzuia kutoka kwa damu kwa mama aliyejifungua, lakini sasa
wengi wanatumia isivyo,” alisema daktari wa magonjwa ya wanawake wa
Hospitali ya Mwananyamala, Taiba Haidar.
Dk Haidar
alisema kwamba wanawake huvitumia vidonge hivyo kienyeji kwa kuviingiza
ukeni au kunywa na matokeo yake wanatokwa damu kwa wingi lakini mimba
yenyewe haitoki na kwamba idadi kubwa ya wanawake wanaotoa mimba hukataa
kusema njia walizotumia hadi pale wanapokuwa mahututi.
“Wakifika hapa huwa wameharibika sana, wengine wanatoka mpaka usaha na wameoza,” alisema
Kuhusu
utomvu wa muhogo, Dk Haidar alieleza: “Ule utomvu wa muhogo una sumu
hiyo ya Oxtoxin, kwa hiyo wakiweka ukeni ule mti unafungua njia ya
kizazi na utomvu unaua kiumbe na mimba inaharibika,” alisema.
Dk
Haidar alisema njia nyingine ni seti ya kusafisha kizazi iitwayo MVA,
ambayo kwa kawaida hutumika kusafisha mimba ya chini ya wiki 12. “Lakini
wapo watu wasio wataalamu wanazinunua hizi na kuzifanyia biashara kwa
kuwatoa wanawake mimba,” alisema na akaiomba Serikali kuzuia uuzwaji
kiholela wa dawa za misoprostol ili kupunguza utoaji wa mimba kienyeji.
Shirika la WHO
Ripoti
ya WHO ya mwaka 2011, inaonyesha kuwa msichana mmoja kati ya wanne
hutoa mimba kwa njia za kienyeji na kati ya mimba 210 milioni
zinazopatikana kila mwaka, 46 milioni sawa na asilimia 22 hutolewa.
Kadhalika, WHO inaeleza kuwa mwanamke mmoja hufa kila baada ya dakika nane kutokana na matatizo ya utoaji mimba usio salama.
WHO
inasema kuwa kati ya hizo, mimba 20 milioni hutolewa kwa njia zisizo
salama na wanawake 70,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na utoaji
wa mimba usio salama.
Utafiti mwingine uliofanywa
nchini na Dk Rose Kipingili na wenzake wa Taasisi ya Afya ya Umma ya
Copanhagen mwaka 2012, umeonyesha kuwa wanawake 751 mkoani Kagera na
Manispaa ya Temeke walitoa mimba kwa njia za kienyeji.
Asilimia
42 ya wanawake walitoa kwa kutumia mizizi ya mitishamba, miti ya mihogo
na majani ya chai huku asilimia 54 walitolewa na watu wasiokuwa na
ujuzi.
Sababu za kutoa
Kwa
mujibu wa madaktari waliohojiwa, miongoni mwa sababu za wanawake kutoa
mimba ni masomo, kupata mimba katika umri mdogo, kupata mimba nje ya
ndoa, kutokuwa tayari kulea mtoto, kuficha watu wasijue kuwa amewahi
kufanya ngono, shinikizo kutoka kwa wanaume au kutotaka kuzaa mtoto
kutokana na mimba iliyotungwa kwa kubakwa.
Baadhi ya
wauguzi na wakunga walieleza hata wanawake walio katika ndoa hufikia
hatua hiyo baada ya kupata mimba wakati wakiwa na watoto wadogo.
Wanasheria
Mwanasheria
wa Chama cha Wanasheria Wanawake nchini (Tawla), Sima Bateyunga amesema
ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni lazima zitafutwe mbinu namna
ya kupunguza pia utoaji wa mimba usio salama kwani unahatarisha maisha
ya mamilioni ya wanawake. Sima alisema ukosefu wa elimu unasababisha
vijana wengi kupata mimba zisizotarajiwa na hivyo kujikuta wakitoa mimba
hizo kwa njia zisizo salama na kuhatarisha maisha yao.
Ofisa
Sheria wa Tawla, Julius Titus anasema bado kuna pengo kubwa kutokana na
kukosekana kwa sheria moja inayoangalia afya ya uzazi.
Post a Comment