Diamond kuburuzwa mahakamani kwa kumtusi Diva


Loveness Malinzi ‘Diva’
NI mtifuano! Agosti 24, mwaka huu ilikuwa siku mbaya kwa nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ au baba Tiffah na mtangazaji anayekimbiza kwa sauti tamu hewani, Loveness Malinzi ‘Diva’ kufuatia kupishana lugha ndani ya studio za redio na hivyo, Diamond kumvurumishia matusi mwenzake.
Kupishana kauli huko kuliashiria kuwepo kwa uhasama wa siku nyingi kwa wawili hao huku kila mmoja akiwa anaamini mwenzake ana makosa na ndipo siri tano za Diamond kumtusi Diva zikajulikana.
MCHEZO ULIVYOANZA
Siku hiyo majira ya saa 9:00 alasiri, Diamond alitia timu kwenye studio za redio hiyo zilizopo Mikocheni, Dar kwa lengo la kumtambulisha msanii wake mpya kutoka studio yake ya Wasafi Records iliyopo Sinza-Mapambano, Dar.Mwanyeji wa Diamond alikuwa mtangazaji Hamis Mandi ‘B12’. Lakini ndani ya studio hiyo alikuwepo Diva.
platnumz
Nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ au baba Tiffah.
ALIANZA DIAMOND
Kabla Diamond hajaanza kumtambulisha msanii wake, alianza na Diva kwa kumsema kwamba amekuwa akimchoresha mitandaoni kwa kumchafua.
DIVA AKAJIBU
Diva alijibu kuwa, kisa cha yeye kumchoresha, aliwahi kumuita Diamond kwenye Kipindi cha Ala za Roho lakini staa huyo hakutokea wakati meneja wake, Salam alimpa taarifa, akakubali na yeye Diva akaanza kutangaza mitandaoni kuwa, siku moja atakuwa na Diamond hewani jambo lilimfanya wasikilizaji wake kusema aliwaongopea na wengine kuanza kumtusi mitandaoni.
DIAMOND ACHAFUA HALI YA HEWA
Baada ya maneno hayo ya Diva, ndipo Diamond apoonesha dalili ya kukasirika na kutoa lugha ya matusi ambayo haiandikiki gazetini lakini akimaanisha kuwa, kama Diva angewahi kuwa mpenzi wake, angemheshimu.
MANENO BILA MPANGILIO
Diva naye alijimjia juu Diamond kwa kumwambia kuwa, hana hadhi ya yeye kuwa mpenzi wake, maneno ambayo yalimchefua baba Tiffah na kuanza kutupiana maneno bila utaratibu hali iliyomlazimisha B12 kuingiza matangazo ili kuwatoa hewani wawili hao.
Baada ya sitofahamu hiyo, Amani lilichimba na kubahatika kuibuka na siri nne (4) zilizomfanya Diamond kumtukana Diva.
SIRI YA KWANZA
Kwanza inadaiwa kuwa, meseji za Diva kwenye mitandao kumsema Diamond kwa kitendo chake cha kutotokea kwenye Kipindi cha Ala za Roho zilimfanya mzazi mwezake, Diamond, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kumbana baba wa mtoto wake huyo akimtaka aseme ukweli kama kuna siri iliyofichika kati yao
“Diamond amekuwa akimkatalia Zari kuwa, hakuna siri wala uhusiano wake na Diva. Kwenye kipindi hicho kama Diamond angekwenda, ilikuwa aongozane na Zari maana alikuwa hajajifungua. Diamond akawa anamwona Diva kama ana lengo la kuvuruga mapenzi yao.
SIRI YA PILI
“Kitendo cha Diva kutumia mitandao kumshambulia, Diamond alikiweka moyoni na kuahidi siku wakikutana laivu atampasulia ya moyoni mwake liwalo na liwe. Hata alipokwenda studio jana (Jumatatu), hakujua kama angekutana na Diva.”
SIRI YA TATU
“Diamond aliamini kuwa, Diva kumshambulia mitandaoni alilenga kumshushia heshima mbele ya jamii ili kumuua kisanii. Maana yeye mwenyewe alisema anaamini maneno ya Diva kwenye mitandao kuna zaidi ya kitendo chake cha kutotokea studio,” kilidai chanzo chetu.
SIRI YA NNE
Kwa upande wake, Diamond alipozungumza na Amani alianika siri ya nne akisema:
“Yule Diva dizaini f’lani kama ananitaka vile lakini mimi simpi nafasi ndiyo maana anatengeneza bifu na mimi.”
DIAMOND ANAENDELEA
“Diva amekuwa akinisema mara kwa mara. Mimi nilikwenda pale kwa lengo lingine, yeye akaanza kuleta zake za kuleta. Kila nikiitafuta sababu siioni. Sijawahi kumkosea popote pale.”
DIVA TAYARI KWA MWANASHERIA WAKE
Amani lilimtafuta Diva juzi kwa lengo la kumsikia anasemaje kuhusiana na sakata hilo ambapo alisema:
“Hii ishu iko kwa wanasheria wangu (tayari kwa kumpeleka Diamond mahakamani). Amenidhalilisha sana kama mwanamke nisiyefaa katika jamii. Ushahidi upo kila kona kwenye mitandao.”
ATISHIWA KUPIGWA, MAISHA
“Akaenda mbali zaidi na kutaka kunipiga maana lugha ya matusi haikutosha. Amenitishia maisha jambo ambalo halitakiwi kisheria. Hakuna aliye juu ya sheria. Sitazungumza zaidi.”
Imeandaliwa na Musa Mateja na Nyemo Chilongani.

Post a Comment

Previous Post Next Post