Simba yaitandika Jang'ombe Boys 3-0 katika mchezo wa kirafiki


 Wachezaji wa timu ya Simba wakipongezana baada ya kuwafunga Jang'ombe Boys
Mfungaji wa moja ya magoli ya Suimba Elia maguri akidhibitiwa vilivyo na beki wa Jang'ombe  Boys

Na Ameir Khalid
ELIAS Maguri ameendelea kutesa kwa kuzifumania nyavu kisiwani Zanzibar, ambako klabu yake Simba SC imekuwa kambini ikicheza mechi za kujipima nguvu.
Jioni hii, Maguri alifunga bao moja wekundu hao wakishinda 3-0 dhidi ya Jang’ombe Boys iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao, katika uwanja wa Amaan.
Simba inayofundishwa na kocha Muingereza Dylon Kerr anayesaidiwa na mzalendo Selemani Matola, ilianza kuzihujumu nyavu za wapinzani wao katika dakika ya 14, Maguri akiwa ndiye mfungaji.
Dakika ya 17, Jang’ombe Boys wakamruhusu Michael Mgimwa kuandika bao la pili, na timu hizo zikaenda mapumziko Simba ikiongoza 2-0.
Simba ilihitimisha ushindi wao kwa bao la dakika ya 81 lililopachikwa kimiani na Samir Omar.
Huo ni mchezo wa nne kwa Simba SC kucheza na kushinda tangu ilipanza kambi yake kisiwani hapa mwanzoni mwa wiki iliyopita, awali ikiifunga kombaini ya Zanzibar 2-1, ikaitandika Black Sailors 4-0, Polisi 2-0 kabla leo kupata ushindi huo wa 3-0 dhidi ya Jang’ombe Boys.

Simba itakamilisha mechi zake Jumatano kwa kupambana na KMKM iliyotolewa hatua za makundi kwenye michuano ya kombe la Kagame iliyomalizika Jumapili, kabla ya kurejea Dar es Salaam Alkhamisi.

Post a Comment

Previous Post Next Post