MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Misungwi, mkoani
Mwanza, imemhukumu msanii wa ngoma za asili, Mng’ahwa Kazanza (42),
kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kumiliki fisi wawili na kuwatumia
kwenye sanaa zake bila kibali.
Awali akisomewa mashtaka katika mahakama hiyo na Mwendesha
Mashtaka wa Polisi, Doroth Mgenyi, ilielezwa mahakamani hapo kuwa mnamo
Septemba 28, mwaka huu, kwenye Kijiji cha Sisu wilayani Misungwi, majira
ya saa 7:30 mchana, Mng’ahwa Kazanza (42) alikamatwa akiwa na fisi
wawili wenye thamani ya Sh milioni 4.8.
Mara baada ya kusomewa mashtaka, msanii huyo alikiri kosa
hilo na kudai alikuwa akiwatumia fisi hao katika sanaa zake bila
kutambua kama ni kosa kuburudisha mashabiki wake kwa lengo la kuongeza
kipato.
Kutokana na kukiri huko, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Ruth Mkisi, alimtia hatiani kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali
kinyume cha sheria Na. 5 ya mwaka 2009 na kumhukumu kwenda jela miaka 10
au kulipa faini ya Sh 4,840,000 ili iwe fundisho kwa watu wengine
wanaomiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria.
Msanii huyo alishindwa kulipa faini hiyo na hivyo kwenda jela kutumikia adhabu hiyo ya miaka 10.
إرسال تعليق