Ni wiki
nyingine tunakutana kupitia ukurasa huu nikiamini uko salama, tayari
kwa kupiga kura keshokutwa kuchagua viongizi watakaotuongoza kwa miaka
mitano ijayo.
Mpenzi msomaji wangu, katika kuifanya
ndoa iwe imara, niliwahi kuzungumzia mavazi sahihi ya mke kumvalia
mumewe wakiwa chumbani. Lakini pia nikasema kwamba, kama kwenye nyumba
mnaishi wawili tu, sioni shida mke kuvaa anavyotaka.
Pia nikasema kuwa, hakuna kitu kibaya
kama mke wa mtu kuvaa nguo zisizo za heshima kwenye nyumba ya kupanga
kiasi cha kuwatega wapangaji wa kiume.
Nilisema hayo baada ya kubaini kuwa,
wapo wanawake ambao wameolewa lakini hawaoni hatari kuvaa kimitego bila
kujali kuwa, kufanya hivyo ni kuiweka rehani ndoa.
Kuna hili vazi la kanga moja ambalo
baadhi ya wanawake wamekuwa wakipenda kulivaa hasa maeneo ya mjini, bila
kujali ni mchana au usiku, kwenye nyumba ya kupanga au binafsi.
Hapo ndipo penye shida na leo nimeona nilizungumzie ili wale wenye tabia hiyo waache mara moja kama wanazitaka ndoa zao.
Niseme tu kwamba, ukiwa na mumeo
chumbani wala sioni tatizo kumvalia kanga moja, wakubwa wanajua faida ya
vazi hili katika kuidumisha ndoa.
Pia ikiwa mnaishi peke yenu, siyo hatari
hata kidogo kuvaa kanga moja, akazurura nayo sebuleni, jikoni na sehemu
nyingine za nyumba yenu. Nasema hivyo kwa sababu, kuvaa minguo kibao
mbele ya mumeo naweza kusema ni ushamba, labda kama kuna baridi sana,
unaumwa au hauko vizuri na mwenza wako. Kinyume chake unaweza kuvaa vazi
hilo na ikawa ni chachu ya mambo yetu yalee.
Shida inakuja pale utakapovaa vazi hilo
kisha kutoka na kwenda bafuni kuoga, mbaya zaidi uwe umejaaliwa umbile
tata kisha kwenye nyumba unayoishi kuna wanaume kibao. Unadhani katika
mazingira hayo ndoa yako itakuwa salama kweli?
Unadhani wapangaji wenzako
watakuheshimu? Sidhani kama itakuwa hivyo. Kwa kuvaa kanga moja ni wazi
utapata usumbufu mkubwa kutoka kwa wanaume wakware na wengi watakuona
unatangaza biashara. Mumeo naye hawezi kufurahia hilo, labda awe ni
miongoni mwa wale malimbukeni.
Unachotakiwa kujua ni kwamba, kuvaa
kanga moja hasa kwa mke wa mtu na kukatiza mbele za wanaume bila aibu ni
kujichoresha. Utadharaulika na hata mumeo hawezi kupata heshima
inayostahili kwani ataonekana kaoa mke mcharuko.
Labda niseme tu kwamba, unatakiwa kuwa
makini sana na mavazi yako. Tambua uvaeje ukiwa na mumeo tu chumbani,
uvaeje ukitoka kwenye geti la nyumba yenu na uvaeje ukiwa ndani ya
nyumba huku ukiwa na familia.
Wapo wanaokosea, unakuta mke wa mtu ana
watoto tena wakubwa tu lakini akiwa ndani kwake anaona sawa kuvaa kanga
moja na akawa anazunguka huku na kule. Hii siyo sawa! Ni kweli wanao
hawawezi kukutamani lakini unawafundisha nini kwa kuvaa hivyo?
Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba,
unapoingia kwenye ndoa unatakiwa kujitofautisha kabisa na wale ambao
wako ‘singo’. Kanga moja ni vazi la kumvalia mumeo tena hasa chumbani.
Usijidhalilishe kuvaa nguo ambayo itakufanya utafsirike tofauti, udharaulike na kuonekana unatangaza biashara wakati una mume.
إرسال تعليق