Hatima ya Juma Duni Haji Kubaki CHADEMA Au Kurudi CUF kujulikana Januari

 


Mwanasiasa mkongwe nchini, Juma Duni Haji amesema hatima yake ya kubakia au kuondoka ndani ya Chadema itajulikana mwezi ujao.
Duni aliihama CUF na kujiunga Chadema ambayo ilimsimamisha kuwa mgombea mwenza wa urais wa Chadema iliyokuwa chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Vyama vingine vinavyounda Ukawa ni NLD na NCCR Mageuzi.
Tangu kuisha kwa Uchaguzi Mkuu na mgombea wa Chadema kushika nafasi ya pili,  Duni amekuwa kimya, lakini juzi alisema itakapofika Januari mwakani ataeleza mustakabali wake kisiasa.
“Kwa sasa sisemi jambo lolote, nitakuambia baadaye kidogo kama nitarudi CUF au nitabakia Chadema. Kuna mambo ninafanya kwanza, nisingependa kusema,” alisema Duni.
Pia, Duni alizungumzia hisia zake za kisiasa visiwani Zanzibar, akisema anashangazwa na kauli ya aliyekuwa Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mark Bomani kumshawishi Maalim Seif Hamad akubali  uchaguzi urudiwe.
Siku chache zilizopita, Jaji Boman alinukuliwa na vyombo vya habari akimtaka Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar kukubali kurudia uchaguzi huo kama ilivyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kuwa utarudiwa ndani ya siku 90.
Jecha alifuta matokeo ya urais na uwakilishi wa Zanzibar, akisema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni na kwamba ndani ya tume yake wajumbe walitofautiana hadi kukunjana.
Jaji Bomani alisema kama Maalim Seif alishinda, atashinda uchaguzi ukirudiwa kwani wananchi watampigia kura.
Hata hivyo, Duni alisema: “Anajua kabisa nchi yoyote inaporudia uchaguzi mara nyingi amani huwa inapotea, kwa mfano Burundi leo hii bado wanauana na hakuna anayezungumza lolote kwa sababu ni chama tawala kimeshinda.
“CUF inasisitiza Katiba ya Zanzibar ilindwe au kwa sababu upande wa Bara wamepata Rais (John Magufuli), sasa hawajali usalama wa Wazanzibari?”
Duni alihamia Chadema chini ya mpango maalumu wa Ukawa wa kuwezesha vyama hivyo kuchukua urais Bara na Visiwani, mpango ambao haukuweza kuzaa matunda.

Post a Comment

Previous Post Next Post