Wema Sepetu na Aunt Ezekiel wamepatana ghafla Mombasa nchini Kenya




 KITUKO! Katika hali isiyotarajiwa, waigizaji wa filamu wenye majina makubwa Bongo, Wema Sepetu na Aunt Ezekiel wamepatana ghafla baada ya ugomvi wao wa muda mrefu.

Katika akaunti zao za mitandao ya kijamii, wawili hao walitupia picha wakiwa pamoja na furaha tele, baada ya hafla ya kukabidhiwa tuzo kwa wasanii zinazojulikana kama Nzumari Awards 2015, zilizofanyika Mombasa nchini Kenya, Ijumaa iliyopita.

Inafahamika kuwa waigizaji hao wamekuwa katika ugomvi mkubwa ambao chanzo chake hakiwekwi wazi, lakini mara kadhaa, wameshindwa kuhudhuria hafla zilizowahusisha wao au familia zao na kwa nyakati tofauti wamekuwa wakipondana.

Chuki kubwa zaidi ya hivi karibuni ni pale Aunt Ezekiel alipompigia ‘promo’ Diamond katika pati yake ya Zari White Party iliyofanyika Mei mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, jambo ambalo lilimkera Wema, aliyetemana na mkali huyo wa kibao cha Mdogomdogo.

Cha kushangaza zaidi, alipoulizwa kama wamepatana lini, Aunt Ezekiel, aliyezaa na dansa wa Diamond, Mose Iyobo alisema; “Kwani tulikuwa tumegombana jamani? Mimi hayo mambo nilikuwa ninasoma kwenye magazeti tu, sisi hatujawahi kugombana hata mara moja.”

Post a Comment

Previous Post Next Post