Gazeti la Mawio lafungiwa maisha




 Sura ya gazeti la mwisho la Mawio kabla ya kufungiwa
BAADA ya kulisakama kwa muda mrefu hatimaye Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nauye, imelifungia kwa muda wote gazeti la kila wiki la MAWIO linalochapishwa na kampuni ya Victoria Media Services Ltd. Anaandika Charles William … (endelea).
Katika tangazo lake lililotolewa kupitia gazeti la Serikali notisi namba 55 ya Januari 15, 2016 Serikali imebainisha kuwa imechukua uamuzi huo wa kulifungia gazeti la Mawio kwa muda wote kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo kupitia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 kifungu cha 25(1).
“Mawio linatakiwa kusimamisha uchapishaji wake kwa kipindi chote ikiwemo pia katika vyombo vya mawasiliano vya kielektroniki kuanzia Januari 15, 2016”, ilisema sehemu ya tangazo hilo ambalo limetolewa katika gazeti la serikali, likisainiwa na waziri Nape Nauye.
Tangazo hilo halikuweza kufafanua zaidi ni makosa gani hasa yaliyosababisha gazeti kufungwa na kwanini adhabu iliyotolewa ni kubwa sana ukizingatia kuwa Mawio halikuwahi kufungiwa wala kuonywa kwa kosa lolote katika siku za wa awali zaidi ya kupokea vitisho kutoka kwa serikali mwanzoni mwa mwezi Januari 2016.
Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa kwa uongozi wa gazeti hilo kupitia Mkurugenzi na Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, Simon Mkina juu ya kufungiwa kwake zaidi ya barua ya msajili wa magazeti iliyoandikwa Januari 6, mwaka huu ikieleza kutoridhishwa na utetezi wa gazeti hilo juu ya uchapishaji wa makala za uchochezi na kuahidi kuchukua hatua.
Serikali ilianza kulikabili rasmi gazeti la Mawio 31 Desemba, 2015 kwa barua iliyoandikwa na msajili wa magazeti ikimtaka mhariri wa gazeti hilo kutoa maelezo ya kwanini gazeti hilo lisifungiwe kufuatia makala zake mbili zenye vichwa vya habari “Hosea kortini” na “Seif Rais Zanzibar” ambazo zilidaiwa kuzua taharuki.
“Nakujulisha kwamba ofisi ya msajili wa magazeti haijaridhika na utetezi wako kwa kuwa hujatoa uthibitisho usio na shaka juu ya madai ya makala ulizochapisha,” ilitamka sehemu ya barua iliyosainiwa na Raphael Hokororo, kwa niaba ya msajili.
Gazeti la Mawio ambalo huandika habari za kiuchunguzi limekuwa likifichua kashfa mbalimbali za ufisadi, uvunjifu wa haki za binadamu na rushwa limefuata mkondo uleule ambao gazeti la MwanaHALISI liliufuata 30 Julai 2012 pale lilipofungiwa kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuchapisha taarifa za uchochezi.
MwanaHALISI lilikaa kifungoni kwa zaidi ya miaka mitatu kabla ya kurejeshwa kwa amri ya Mahakama Kuu mwezi Agosti, 2015 kufuatia Mkurugenzi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea kufungua kesi, akipinga kufungiwa kwa gazeti hilo.
Mpango wa kulifungia gazeti hilo ulitajwa kubainika mapema kufuatia kurejeshwa kwa gazeti la MwanaHALISI mnamo mwezi Agosti, 2015 na hivyo serikali kupitia msajili wa magazeti kutokuwa tayari kuvumilia machapisho ya habari na makala za kiuchunguzi kila wiki kutoka katika magazeti hayo na hivyo kutafuta namna ya kulifungia mojawapo.
Mkurugenzi wa kampuni ya Victoria Media Services Ltd ambaye pia ndiye Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mawio, Simon Martha Mkina, amelaani vikali kitendo cha serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kuanza kuminya uhuru wa vyombo vya habari na kujaribu kuzima sauti za wanyonge hapa nchini.
“Serikali lazima iwe na uvumilivu wa kusikia na hata kuona isiyoyapenda, ilimradi ni kilio cha wananchi wake, MAWIO limekuwa gazeti pekee linalobeba kilio hicho, ni njia ya wasiokuwa na sauti kusikika. Sasa wamezibwa midomo-wakasemee wapi? Ni ubabe.” Inaeleza sehemu ya taarifa ya Mkina aliyoitoa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

CHANZO: MWANAHALISI ONLINE 

Post a Comment

Previous Post Next Post