Waziri Kitwanga Aanika Siri Ya Kutumbuliwa Kwa Vigogo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)


Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) waliokumbwa na ‘operesheni tumbua majipu’, walikutwa na mali nyingi “kupita maelezo”, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.

Operesheni hiyo, ambayo inatekelezwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, juzi ilimkumba Dickson Maimu, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Nida, Joseph Makani (Mkurugenzi wa Tehama), Rahel Mapande (Ofisa Ugavi Mkuu), Sabrina Nyoni (Mkurugenzi wa Sheria) na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hatua ya kutengua na kusimamisha watumishi hao imechukuliwa baada ya uchunguzi wa hali ya juu kwenye mamlaka hiyo.

Ingawa hakutana kuingia kwa undani akihofia kuingilia uchunguzi, Kitwanga alisema katika uchunguzi wao, moja ya hatua ilikuwa ni kukamata mali za wafanyakazi hao wa  Nida.

“Walipoulizwa, walisema wamepata mali hizo kutokana na mikopo, hivyo uchunguzi utajielekeza katika kulinganisha kiwango cha mikopo na mali walizonazo,” alisema.

Waziri huyo alisema uchunguzi zaidi unajielekeza katika ni jinsi gani Sh180 bilioni zilitumika kusajili watu milioni sita tu na kati yao kuwapata vitambulisho watu milioni 2.5 tu.

“Ninayo taarifa niliyopewa na Nida ikionyesha kwamba imepanga ofisi nyingi Dar es Salaam zisizo na matumizi na wakati fulani walinunua ‘seva’ 100 zisizo na matumizi,” alisema.

“Haielezeki, NEC ilitumia kiasi kama hicho kuandikisha watu milioni 20 katika miezi isiyozidi mitano, lakini Nida wametumia Sh180 bilioni kuandikisha watu milioni 2.5 kwa miaka mitatu.”

Mbali na kuwaweka kando watendaji hao, Rais aliagiza vyombo mbalimbali kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha katika mamlaka hiyo.

Vyombo vilivyoagizwa ni pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi ya Umma (PPRA).

No comments:

Post a Comment