Mkemia Mkuu kubaini waliozaliwa na jinsi mbili na kueleza ni ipi jinsi tawala yenye nguvu zaidi

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali itakuwa na uwezo na mamlaka ya kuchunguza watu waliozaliwa na jinsi mbili na kubaini jinsi tawala yenye nguvu zaidi. 3019942-poster-p-the-marketing-challenge-of-99-dna-testing-company-23andme
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016, uliopitishwa juzi usiku saa nne bungeni unampa Mkemia Mkuu mamlaka ya kuchunguza na kubaini jinsi ya mtu na kutatua utata kwa mtu atakayekuwa amezaliwa na jinsi mbili.
“Waheshimiwa wabunge naona wengi wenu mnadhani mkemia mkuu kazi yake ni kuchunguza vinasaba kubaini uhalali wa mzazi na mtoto, maana naona wabunge wengi wamelishabikia hilo, lakini katika teknolojia ya vinasaba yanahusu pia utambuzi wa jinsi, watu unakuta wanawake au wanaume wanazaliwa jinsi ya kike na kiume, kwa hiyo tunaangalia jinsi tawala ni ipi ina nguvu,” alisema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Ummy alikuwa akijibu michango ya wabunge waliochangia wakati wa kujadili Muswada wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 kabla ya kuupitisha juzi usiku, waliotaka mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu kutoa elimu kwa wananchi juu ya shughuli zake.
Alisema kwa sheria hiyo, sasa mkemia mkuu kupitia maabara yake anaweza kusema jinsi ya kike au ya kiume ndio yenye nguvu, lakini pia kuna suala la kuhakikisha utambuzi wa mwanadamu hasa wakati yanapotokea majanga pamoja na watu wanaosafiri kwa makundi.
Alikubaliana na wabunge kuwa iko haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya kazi za maabara ya mkemia mkuu ambao wengi wao wanadhani inafanya kazi hiyo tu ya kubaini vinasaba vya mzazi na mtoto, lakini sasa wafahamu hata waliozaliwa na jinsi mbili wanaweza kutegua utata huo kwa kubaini jinsi tawala au jinsi yenye nguvu zaidi kama ni ya kiume au ya kike

No comments:

Post a Comment