Polisi Arusha yatoa onyo kwa wanaolima bangi

Jeshi la Polisi mkoani hapa lipo kwenye mkakati wa kuwachukulia hatua viongozi wote wanaoishi au kufanyia kazi katika maeneo ambayo yatabainika wananchi wa maeneo yao wanalima bangi bila wao kuwachukulia hatua zozote au kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu kamishna (DCP) Charles Mkumbo alipokuwa anaongea na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya operesheni iliyofanyika katikati ya wiki iliyopita katika kijiji cha Kismiri Juu, kata ya Uwiro tarafa ya King’ori wilayani Arumeru,
“Mara kadhaa tunapofanya operesheni hizo wananchi wa eneo hilo huwa wanakimbia na kuacha nyumba zao huku viongozi wao kutoonekana kabisa au kutoa taarifa zozote juu ya uhalifu huo, sasa tutawachukulia hatua kwani wao ni sehemu ya uwajibikaji katika kuzuia vitendo vya uhalifu”. Alisema Kamanda Mkumbo.
jc9a3527Mkuu wa Kikosi cha kutuliza Ghasia mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Ramadhani Giro akiwa anaonyesha burungutu la madawa ya kulevya aina ya bangi ambalo lilikuwa limehifadhiwa kwenye moja ya magunia yaliyopatikana katika kijiji cha Kismiri Juu wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Katika operesheni hiyo, jeshi la Polisi lilifanikiwa kupata jumla ya magunia 22 ya bangi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba za wakazi hao na kwenye makorongo yanayozunguka kijiji hicho pamoja na kilogramu 80 za mbegu za mmea huo ambazo zote ziliharibiwa kwa kuchomwa moto.
Kamanda Mkumbo aliendelea kueleza kwamba, katika operesheni hiyo pia walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye Raphael Laizer (33) mkazi wa Kismiri Juu akiwa na magunia matatu ya bangi huku taratibu za kumfikisha mahakamani zikiwa zinaendelea.
jc9a3541Mkuu wa Operesheni mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James Manyama akiwa ameshikilia ndoo lenye mbegu za mmea wa bangi mara baada ya operesheni iliyofanywa na jeshi la Polisi kijiji cha Kismiri wilayani Arumeru kumalizika. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Kamanda Mkumbo aliongeza kwa  kusema kwamba, imekuwa vigumu kuwakamata watuhumiwa kutokana  na  jiografia ya eneo hilo ambapo kila kunapokuwa na operesheni askari wanapokwenda,  wananchi hao wanawaona kirahisi au kusikia miungurumo ya gari na kisha hukimbilia milimani na kuwaacha wazee na watoto.
“Japokuwa operesheni hizo ambazo tunazifanya mara kwa mara zimekuwa za mafanikio lakini changamoto zilizopo ni pamoja na miundo mbinu ya eneo hilo si rafiki kwa magari hasa uwepo wa milima mirefu na ubovu wa barabara”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
Operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka saa 7:30 mchana ilijumuisha askari wa vikosi na vitengo mbalimbali huku ikisimamiwa na Mkuu wa Operesheni mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James Manyama.
jc9a3556Mmoja wa askari wa Jeshi la Polisi akiwa anaendelea na zoezi uchomaji wa bangi katika kijiji cha Kismiri Juu, wilayani Arumeru wakati wa operesheni iliyofanyika katika eneo hilo.
jc9a3577Askari wa Jeshi la Polisi wakivusha moja ya gunia la bhangi lililofichwa katika korongo wakati wa operesheni ya bangi iliyofanyika kijiji cha Kismiri wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Post a Comment

Previous Post Next Post