TUHUMA: SIMBA NA YANGA ZATUHUMIWA KUTUMIA PESA KUIHARIBIA AZAM

KASHFA nyingine imezikumba klabu za Simba na Yanga zikidaiwa kuanzisha kampeni ya kutoa fedha kuhakikisha Azam haipati ubingwa msimu huu ambayo inaitwa 'kampeni didimiza Azam'.

Azam inaonekana kuwa tishio katika harakati za Simba na Yanga kuendelea kutawala soka ya Tanzania kwenye miaka ya karibuni.

Habari ambazo Mwananchi ilizipata zinadai kuwa viongozi wa Simba na Yanga walifanya kikao mwezi uliopita kwenye Hoteli ya Kempinski na kukubalina kwamba watahakikisha Azam haichukui ubingwa msimu huu.

Chanzo hicho kilidai kuwa viongozi hao walikubaliana kutumia mbinu zote kuhakikisha Azam haipati ubingwa, pia waliafikiana kutofanya michezo michafu katika michezo yao.

Mwananchi ilipomtafuta Katibu wa Simba, Evodius Mtawala kujibu tuhuma hizo alisema hana taarifa za kikao hicho cha pamoja na kwamba ndiyo kwanza anazisikia habari hizo.

"Sijawahi kusikia kikao kama hicho ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako, sijui lolote," alisema Mtawala.

Naye Katibu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema, "Sielewi taarifa hizo kwani ni siasa ambazo nimekuwa nikizisikia kila wakati hivyo sishangazwi nazo zaidi ya kuangalia majukumu yangu ya kazi yanayonikabili."

"Hivi hizo habari mnazipata wapi? Kikao kama hicho ndiyo nakisikia kwako, hakuna taarifa hizo na wala sijasikia tuhuma kama hizo ambazo mimi naziita ni siasa za soka, acha timu zicheze, ni mapema sana kuanza kuzungumza mambo kama hayo ambayo mimi binafsi siyapi nafasi," alisema Mwalusako.

Hata hivyo chanzo chetu cha habari kilidai kuwa,"Kampeni hiyo imeingia dosari hivi karibuni baada ya viongozi wa Simba kudaiwa kutoa fedha kwa Kagera Sugar walipokuwa wanacheza na Yanga ili wawafunge."

"Tumebaini baada ya hapo viongozi wa Yanga nao wameapa kulipiza kisasa kwa Simba kwa kuhakikisha wanapitisha mikono yao kwa kila mechi watakayocheza ili wasiweze kutetea ubingwa wao," alisema kiongozi huyo aliyedai kuwa alishiriki katika kikao hicho ambaye ndiyo chanzo chetu cha habari hii.

Katika hatua nyingine chanzo hicho kilidai kuwa Azam katika kujihami imeingia katika mchezo mchafu wa kutoa fedha ili watwae ubingwa wa ligi baada ya msimu uliopita kuishia katika nafasi ya pili.

Yanga wanadaiwa walitoa ahadi ya Sh10 milioni kwa wachezaji wa Kagera Sugar kama wangeifunga Simba juzi, lakini kwa sare hiyo vijana wa Kagera walikabidhiwa Sh5 milioni huku Azam wakishutumiwa kutoa Sh7milioni kwa waamuzi wa mchezo huo ili kuwakandamiza Simba.

Akizungumzia tuhuma hizo, mratibu wa timu ya Azam, Patrick Kahemela alisema hawajawahi kutumia fedha ili kuharibu mechi ya Simba.

"Hatuna taarifa zozote juu ya kufanyiwa fitina hizo zaidi ya kuangalia malengo yetu ya kutwaa ubingwa kwa kucheza soka la uwanjani," alisema Kahemela.

Hivi karibuni Kocha wa Kagera Sugar, Abdallah Kibaden aliilamikia TFF kwa kushindwa kuchukua hatua ya kupambana na rushwa michezoni.

"Kutokana na baadhi ya waamuzi kuhongwa fedha na kupindisha sheria za soka, siku zote matokeo huwa mabaya na yasiyotarajiwa," alisema Kibaden.
(Source: www.mwananchi.co.tz)

Post a Comment

أحدث أقدم