Ulimboka Kutaja Wabaya Wake


KIONGOZI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka, amepanga kumwaga taarifa nyeti kuhusu kutekwa na kuteswa kwake na kisha kutupwa katika Msitu wa Mabwepande, Bunju, jijini Dar es Salaam. 

 Mmoja wa ndugu na rafiki wa karibu wa Dk Ulimboka, ameliambia Mwananchi kuwa, kiongozi huyo wa jumuiya, amepanga kuanika hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari. Alisema Dk Ulimboka, atatumia mkutano huo kueleza siri ya kutekwa kwake.

 “Siku yoyote kuanzia sasa umma, utafahamu ukweli halisi wa kilichompata kijana wetu. Niliongea naye juzi na amenithibitishia kuwa atakutana na waandishi wa habari na kueleza kila kitu katika masahiba yaliompata,” alisema ndugu huyo wa Ulimboka ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake litajwe gazetini. 

Alisisitiza “Ni kweli kwamba Steven (Dk. Steven Ulimboka) amepanga kukutana na waandishi wa habari. Anataka kutumia mkutano huo, kuanika wote walioshiriki kumtesa, kumteka na kisha kumtupa katika msitu wa Mabwepande,” Alipoulizwa kuhusu kipya ambacho daktari huyo ataueleleza ulimwengu ambacho hakijafahamika, mwanafamilia huyo alisema: 

“Tuvute subira. Steven amepanga kutaja wote waliohusika katika kutaka kuangamiza maisha yake. Ameniambia kuwa anataka kuwaambia Watanzania ukweli wa kilichompata,” Dk Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26 mwaka huu, katika maeneo ya Leaders Club jijini Dar es Salaam na baadaye kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikononi na miguuni kabla ya kunyofolewa kucha na meno; katika Msitu wa Mabwepande. 

Aliokotwa na wasamaria wema asubuhi yake na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alilazwa kabla ya kupelekwa Afrika Kusini Juni 30 kwa matibabu zaidi. Tangu aliporejea nchini Agosti 12 mwaka huu, kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka ndani na nje ya nchi, kumtaka azungumze kwa madai kuwa kauli yake itasaidia kujulikana kwa ukweli kuhusu kilichompata. Kufanyika kwa mkutano huo kunatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa kunaweza kuondoa kiwingu hicho, ikiwa ni pamoja na kujibu baadhi ya maswali yaliyobuka juu ya tukio hilo. 

mahojiano yake ya kwanza na gazeti hili, wiki iliyopita, Dk. Ulimboka alisema hali yake inaendelea kuimarika siku hadi siku na kwamba anamshukuru Mungu na wote waliomuombea, ingawa bado anahitaji matibabu zaidi. 

“Madaktari wangu bado wanaendelea na uchunguzi kuhusu figo zangu ili waone kama zinaweza kufanya kazi au zinahitaji kuondolewa na kuwekwa nyingine. Lakini kwa jumla, hali yangu inaleta matumaini kidogo.

Post a Comment

أحدث أقدم