Mkuu
wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, akimtunza Mmoja wa wasanii wa
Jeshi la JKT Mgambo, waliokuwa wakitoa burudani katika la Utamaduni
Handeni.(Picha na mpiga picha wetu).
Wasanii
wa ngoma za asili kutoka JKT Mgambo, wakitumbuiza Mamia ya Wananchi
waliofika katika Tamasha la Utamaduni Handeni, sherehe hizo zilifanyika
katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, Mkoani Tanga.
Kikundi
cha Sarakasi kutoka JKT Mgambo wakionesha uwezo wao katika Tamasha la
Utamaduni Handeni, Tamasha hilo lilifanyika mwishoni mwa juma, katika
uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, Mkoani Tanga.
Na Mwandishi Wetu, Handeni
MSIMU
wa kwanza wa Tamasha la Utamaduni wilayani Handeni, mkoani Tanga,
(Handeni Kwetu 2013), lililokuwa likisubiriwa kwa hamu hatimaye
lilifanyika mwishoni mwa juma, wilayani hapa ambapo Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilijitokeza na kudhamini, hivyo kulifanikisha
kwa kiasi kikubwa mno.
Shirika
hilo, likiwa limejitokeza dakika za mwisho katoa udhamini wake katika
tamasha hilo kubwa na la kwanza kuwahi kufanyika katika Ardhi ya wilaya
ya Handeni linalojumuisha vijiji zaidi ya kumi, lilichangia fedha
taslimu shilingi milioni mbili, fedha ambazo kwa kiasi kikubwa ukiacha
mchango wa wahisani wengine zilichangia kufanikiwa kwa Tamasha hilo.
Akizungumza
wakati wa kutambulisha wadhamini na wahisani mbalimbali waliofanikisha
kufanyika kwa Tamasha hilo, mratibu wa Tamasha la utamaduni Handeni
2013, Kambi Mbwana alisema udhamini wa NSSF ulikuwa mkombozi mkubwa
kwao.
“Awali ya yote napenda kutanguliza shukrani zangu zote kwa wahisani wa
tamasha hili, hasa ndugu zetu wa NSSF maana hakika wameonyesha moyo wa
uungwana katika kuhakikisha kuwa Handeni Kwetu inazaliwa kwa mafanikio,
ukizingatia kuwa tamasha hili limekusanya watu wa aina mbalimbali.
Awali
akizungumza baada ya kuzindua Tamasha hilo ambalo lengo lake lilikuwa
ni kuwakutanisha watu wa Handeni kusherekea utamaduni wao pamoja na
kukumbusha umuhimu wa kujenga Handeni, Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya
Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema kwa kuwa na Matamasha kama hayo
jamii inaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kupata Maendeleo wanayoyataka.
Muhingo
alisema ili mafanikio yapatikane katika kila jambo ni lazima watu wa
eneo fulani wawe na utayari wa kukutana na kujadili mambo yao kwa sauti
kama waratibu wa tamasha hilo walivyofanya.
“Tunajivunia
kuwa na vijana wenye mawazo mapana kama haya, naambiwa tamasha hili ni
matokeo ya mawazo ya kimaendeleo ya vijana wetu, hongereni sana,”
alisema Rweyemamu.
Kwa
upande wake, Meneja wa NSSF, mkoani Tanga, Frank Maduga alisema shirika
hilo limedhamiria kuendelea kushirikiana na waaandaaji wa tamasha hilo
kwa lengo la kuhakikisha Utamaduni wa Mtanzania unatumika kulitangaza
Taifa, pamoja na kutumia fursa hiyo kuchangia shughuli za kimaendeleo
kwa kutoa elimu ya huduma zao wilayani Handeni na Tanzania kwa ujumla.
“NSSF
ni shirika la Watanzania na tumedhamiria kuwapatia huduma bora
Watanzania wote, hivyo kila mtu ana haki ya kujiunga na mfuko huu kwa
ajili ya kujiwekea mazingira mazuri katika wakati wote wa maisha yake,”
alisema Maduga.
Katika
tamasha hilo,kulikuwa na vionjo mbalimbali vya Utamaduni wa
Wanahandeni, ikiwa ni Pamoja na Ngoma za asili kutoka katika Vijiji vya
wilaya ya Handeni kama vile, Kweingoma, Kwamatukutu, Kwediamba, Kwachaga
pamoja na vikundi vingine vya Handeni Mjini.
Burudani
kali na ya kuvutia iliyoonesha asili kamili ya Mtanzania ilitoka kwa
Kundi la Sanaa la Jeshi la JKT Mgambo, Azimio Jazz band bila kusahau
msanii wa kundi la Fataki, Machenja ambaye alipiga onesho la kukata kiu
akiwa na wana okalandima.
Tamasha
la Utamaduni Handeni ambalo linafanyika kwa mara ya Kwanza
lilidhaminiwa na NSSF, Clouds FM, Vodacom, Plan B, gazeti la Mwananchi,
Kajunason Blog, Chichi Local Wear, Katomu Solar specialist, Dullah Tiles
and Construction, Anesa Company Limited, Country Business directory,
Jiachie Blog na Taifa Letu.com.
إرسال تعليق