KING KIBADENI MPUTA ARUDISHA MAJESHI SOKA LA VIJANA

WINGA machachari na kocha wa zamani wa Simba sc, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Abdallah Kibadeni Mputa’ amesema hataki tena presha ya kufundisha klabu za ligi kuu soka Tanzania bara.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mtandao huu, Kibadeni aliyeiongoza Simba mzunguko wa kwanza msimu uliopita kabla ya kurithiwa na Zdravko Logarusic alisema anajenga akademi yake maeneo ya Chanika jijini Dar es salaam ambapo atakuwa anafundisha soka vijana wadogo.
Akademi hiyo itakayojulikana kwa jina la ‘Kibadeni Soccer Academy’, KISA itakuwa inachukua vijana kutoka maeneo mbalimbali.
Kibadeni mwenye rekodi ya pekee ya kufunga mabao matatu ‘Hat-trick’ katika mechi ya watani wa jadi mwaka 1977 ambayo haijavunjwa mpaka leo alisema amechoshwa na dharau za baadhi ya wadau wa michezo hasa wanaposema hajasomea mpira wakati alikwenda Ujerumani na Brazil kupiga shule.
Akizungumzia mechi ya watani wa jadi Oktoba 18 mwaka huu, Kibadeni mwenye rekodi ya pekee Afrika mashariki na kati kwa kuifikisha Simba fainali ya kombe la CAF mwaka 1993 alisema ni mechi ngumu, timu itakayocheza kwa umakini itaweza kushinda, lakini hawezi kutabiri matokeo.
Hata hivyo alishangazwa na sare tatu walizopata Simba katika mechi tatu za kwanza akisema haoni sababu ya matokeo hayo kwasababu wamesajili wachezaji wakali.
“Sielewi kinachowakumba, kwa uongozi thabiti walionao, usajili waliofanya, nashangaa kuona wanapata matokeo kama haya. Nadhani kuna sehemu wamekosea, labda kuna watu wanawaombea dua mbaya kwasasa waliwafanyia vitu vibaya”. Alisema Kibadeni.

Post a Comment

أحدث أقدم