Hayo ndiyo yaliyotukia katika sinema hii ambayo kimsingi
inataka kuwashawishi watu kuwa waangalifu katika maelezo na maamuzi yao.
Pamoja na nusu ya sinema kuonesha uchizi unaomkuta mtu baada
ya maamuzi mabaya dhidi yake katika mapenzi, waigizaji waliweza kuchukua nafasi
ya kutenda vyema japo uchukuaji picha unaweza kuwa na walakini.
Naam, ni filamu ambayo inaanza na dhiki kubwa na kumalizwa na
dhiki hiyo hiyo kama vile mhusika wake amepigwa laana.
Katika sinema hii kijana Dick anatimuliwa katika kazi yake
kiwanda cha matofali kwa dai la kuwa yeye ni mwizi japokuwa alisaidia kuimarika
kwa kiwanda hicho tangu awali. Kosa lake kubwa unaweza kusema ni kuwawezesha
jamaa zake kuajiriwa hapo na hao hao wakamtengenezea fitna iliyomtoa kazini.
Baada ya kutoka kazini akabaki nyumbani hoi kiakili, atafanya
nini wakati maisha ni mabaya akiwa na mdogo anayemtegemea achange karata ili
aweze kuendelea na shule? Baba naye uwezo hana.
Rafiki yake Emma anamtuliza kwamba yeye ni mwanaume na anaweza
kupata kazi.Anaenda kwa rafiki yake wa kike pia anamliwaza. Kijana anaendelea
kutafuta kazi lakini ndiyo hivyo tena!
Akiwa bado hana kazi, rafiki yake wa kike anamwambia anahitaji
gauni la harusi kwa ajili ya harusi ya mdogo wake. Jamaa anasema hawezi, lakini
anashawishika na anakubalika na jamaa anahaha mitaani kutafuta fedha za gauni
la harusi ili mpenziwe akamsimamie vyema mdogo wake.
Siku ya harusi mchiriku unapigwa, tahamaki anayeolewa ni
mchuchu wake jamaa anaanguka na kuzimia. Anapoamka akili imepata taharuki
haamini akaishia kuwa nusu mwehu nusu mwenye akili.
Anakuwa mvuta bangi, anajidunga anapora, system nzima inakuwa
imevurugika na mwishoni mwa siku anakuwa
mtu anayehitaji msaada zaidi.
Baba anchanganyikiwa, mdogo mtu anachanganyikiwa na habari zinapomfikia
mhusika na tibutibu hilo anajikuta akiwaza afanye nini. Anakuja kubaini kwamba
ameharibu, amelikoroga na hawezi kulinywa baada ya juhudi ya kutaka kulinywa
kikombe kupasuliwa na baba yake Dick aliyewatoa baruti yeye na rafiki yake kwa
panga.
Kule alikoenda kuolewa mwali Yule, mambo hayakuwa mambo, jamaa
alikuwa kipanga na alikuwa ana wapanga wanawake kama vile mashati katika
maduka.
Mume hakuwa mume, alikuwa kumbe analipiza kisasi kwa wanawake
kwa kujikuta anaukimwi. Binti
alipogundua kwamba kumbe naye kaachwa na ukimwi anahaha lakini mwishoni mwa
siku anarejea nyumbani anaandika barua kwa mpenzi wake wa zamani, teja na
kumtaka radhi kwa kuvuruga penzi halisi.
Anamwachia nyumba na kila kitu ambacho alitakiwa kukimiliki
baada ya mume yule kuondoka kwenda kuendeleza libeneke lake kwingine huku
akimwachia hati ya nyumba na kila kitu.
Kabla hajaondoka jamaa alimwambia alifanya hivyo na ataendelea
kufanya hivyo kwa kila mwanamke atakayejipendekeza kutaka hela kwake kama
sehemu ya maisha yake yaliyobaki.
Sinema hii inamalizika bila kuonesha suluhu ya dhiki, ni kwa
teja Yule kusema neno la mshangao.
Je ujumbe umefika?
Ujumbe gani? Ujumbe wa moyo ukipasuka unakuwa na matatizo? Yes kwani wa kuutibu
ni Yule Yule aliyeupasua. La msingi ni kuwa maamuzi yetu yasiwe na pupa na
lazima tuone nini kitatokea baada ya maamuzi na kuona kama matokeo hayo ndiyo
tunayotaka.
Kwa maana mdada kwenye sinema hii alitaka kununuliwa gauni iwe
mwisho wa mapenzi yake na Dick lakini kumbe ndio akaja kugundua kwamba Dick
alimuona yeye ni kila kitu na alipovuruga nay eye akavurugika.
Maleba na muonekana wa Dick kwa sinema nzima ni wa kichizi
zaidi kuliko teja, mateja wengi ni nadhifu au kwa kuwa Dick alishaanza maisha
kwa dhiki? Mtengeneza sinema ndiye mwenye majibu mimi nimefanya kuandika tu
kuhusu hadithi hii.
Washiriki ni Rakheem David 'Kuch Kuch(aliyekuwa anasambaza
miwaya) Salma Goha ,Sadik Senya pamoja
na Mohamed Fungafunga.
mwisho
إرسال تعليق