Zanzibar: Wanasheria na wanasiasa Zanzibar,
wameunga mkono msimamo wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
wa kupinga kampeni ya hapana kupinga Katiba iliyopendekezwa kupitishwa
na wananchi kwa sababu imelenga kufuta hadhi ya Zanzibar kuwa nchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana mjini
Zanzibar, wanasheria na wanasiasa hao walisema hatua ya Maalim Seif
kupinga Katiba hiyo ni haki yake kwa mujibu wa sheria kama kiongozi au
mtu binafsi.
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh
Ali Said alisema anaunga mkono msimamo wa Seif kwa sababu Katiba
inakuja kuondoa hadhi ya Zanzibar kuwa nchi na mamlaka ya kikatiba ya
Rais wa Zanzibar ya kugawa mipaka ya wilaya na mikoa yake.
“Bahati mbaya tangu kupatikana kwa Uhuru,
Watanzania hawajawahi kuwa na Katiba inayotokana na wananchi bali
wamekuwa wakiongozwa na Katiba zinazotokana na watawala wa Zanzibar na
Tanzania Bara,” alisema Awadhi.
Upande wake, mwanasheria mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamid Mbwezeleni alisema kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni.
“Suala la kukubali au kukataa Katiba ni haki ya
kila mtu, wanasiasa wakae kando wasiamue mambo kwa niaba ya wananchi...
wananchi waisome Katiba iliyopendekezwa kabla ya kura ya maoni,” alisema
Mbwezeleni.
Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatibu alisema msimamo wa Maalim Seif ni muafaka kwa sababu suala la Katiba ni la kila mtu
Hata hivyo, alisema kama Katiba iliyopendekezwa
imeonekana kutozingatia masilahi ya Zanzibar, basi Wazanzibari wenyewe
ndiyo wa kulaumiwa kutokana na kupata fursa nzuri na kushindwa kuitumia
kwa kutetea misimamo ya vyama badala ya masilahi ya Zanzibar na wananchi
wake.
“Sisi tumepata fursa nzuri, bahati mbaya
tumeshindwa kutumia vizuri kwa kutetea misimamo ya vyama badala ya
masilahi ya Zanzibar na watu wake.” alisema Khatibu ambaye alikuwa
mjumbe wa Bunge la Katiba.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق