Spika wa bunge Mh Anna Makinda amesema siyo jukumu lake kuwaondoa
wenyeviti wa kamati za bunge ambao wanatuhumiwa katika sakata la akaunti
ya Tegeta Escrow isipokuwa wao wenyewe wanatakiwa kutii azimio la bunge
namba tatu linalowataka wajiuzulu.
Wakati Mh Makinda akieleza hayo tena kwa kusisitiza kuwa wenyeviti
hao tayari wameshajiuzulu baadhi ya kamati ikiwemo ya katiba na sheria
ambayo mwenyekiti wake ni Mh William Ngeleja ambaye ni miongoni mwa
wabunge wanaotuhumiwa kwenye sakata hilo bado anaendelea na wadhifa huo.
Mh Makinda ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu maswali ya waandishi
wa habari mara baada ya kupokea msaada wa vifaa vya Teknohama
vilivyotolewa na serikali ya China kupitia balozi wake hapa nchini
ambapo amesema vifaa hivyo vitaweza kuokoa zaidi ya bilioni moja ambazo
hutumika kuchapisha miswada mbalimbali na taarifa nyingine za bunge
badala yake sasa wabunge watakuwa wanatumiwa moja kwa moja kwenye
mtandao.
Akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya dola za kimarekani laki
moja balozi wa china hapa nchini Lu Youqing amesema vifaa hivyo ni ahadi
aliyoitoa rais wa China wakati wa ziara yake hapa nchini ambapo
alimwahidi spika wa bunge Mh Makinda na kuongeza kuwa china imewekeza
zaidi ya dola bilioni 3.1 hasa sekta ya kilimo na viwanda na kwamba kuna
kampuni zaidi ya 500 zinazomilikiwa na wachina ambazo zimetoa ajira kwa
watanzania laki moja.
- ITV
إرسال تعليق