Dar es Salaam. Rais Joachim Gauck wa Ujerumani ameambatana na
ujumbe mzito wa wafanyabiasha 14 katika ziara yake ya siku tano nchini.
Rais huyo aliyewasili jana usiku nchini
atazungumzia fursa za uwekezaji katika kilimo, biashara na usarifishaji.
Pia kuhusiana na mradi wa uzalishaji wa mbolea unatakaofanywa baina ya
Kampuni ya Ferrostaal GmbH pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli
nchini (TPDC), yenye uwezo wakuzalisha mbolea tani 1.3 milioni kwa
mwaka.
Akitoa taarifa ya ujio wa rais huyo jana, jijini
Dar es Salaam, balozi mdogo wa Ujerumani nchini, John Reyels alisema
baada ya kuwasili, kiongozi huyo atakuwa na mazungumzo ya faragha na
Rais Kikwete ambayo yatalenga mambo mbalimbali ikiwamo suala la
uwekezaji.
Licha ya kuwa, Balozi Reyels hakufafanua zaidi
kuhusiana na kile atakachozungumza Rais Gauck, lakini alisema kuwa
kupitia wajumbe 14 ambayo ni wafanyabiashara wakubwa wa nchini humo
wataangazia fursa za uwekezaji nchini na mradi huo unaotarajiwa
kutekelezwa kati ya 2019/2020.
Wajumbe hao ni kati ya wajumbe 90 waliyoongozana
na Rais Gauck katika ziara yake nchini ambayo ataifanya kwa siku tano na
kurejea Ujerumani.
Rais huyo, ambaye anatembela Tanzania kwa mara ya
kwanza kutokana na mwaliko wa Rais Kikwete, pia atatembelea Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front.
“Wakati ziara yake kanisani hapo Rais Gauck
atakuwa na mazungumzo na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Alex
Malasusa,”alisema Balozi Reyels.
Balozi Reyels, alieleza sababu ya Rais huyo
kutembelea kanisa hilo na kusema kuwa, “Kanisa hilo linahistoria kubwa
na Ujerumani kwani lilijengwa na Wajerumani takriban miaka 100
iliyopita…hata hivyo Rais mwenyewe aliwahi kuwa mchungaji kabla ya kuwa
na wadhfa alionao sasa”
إرسال تعليق