Mahalu hana hatia - mawakili

MAWAKILI wanaomtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Prof. Costa Mahalu, na Meneja Utawala na Fedha, Grace Martin, wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, awaachie huru katika kesi ya wizi wa euro milioni tatu kwa madai kuwa upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kama walitenda makosa hayo.
Balozi Mahalu aliwasilisha maombi hayo jana mchana kupitia mawakili wake Mabere Marando, Beatus Malima, Alex Mgongolwa na Cuthbert Tenga kwa njia ya maandishi kama walivyoamriwa kufanya hiyo na Hakimu Mfawidhi Ilvin Mugeta.
Kwa mujibu wa maombi hayo, mawakili waliikumbusha mahakama kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita likiwemo kosa la kula njama, za kuiba euro milioni mbili, kughushi vocha za manunuzi ya jengo la ubalozi, kutumia risiti za manunuzi kuidanganya serikali, kuisababishia serikali hasara ya euro milioni 3.
Kwa mujibu wa hoja zao tano muhimu ambazo wamezitumia kuwasilisha ombi hilo, kwanza wanasema serikali ilimruhusu Mahalu kununua jengo la ubalozi kwa njia ya mikataba miwili kwa bei ya euro 3,098,741.58 na kwamba alileta vielelezo kadhaa ambavyo viliweza kuithibitishia mahakama hiyo kuwa serikali iliridhia jengo hilo linunuliwe.
Walisema kuwa hakuna ushahidi wowote ulioletwa na upande wa jamhuri kuwa washtakiwa walifanya siri na kutenda kosa la wizi na katika hoja ya pili walisema kuwa upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha muuzaji wa jengo hilo kuwa hakupokea fedha hizo euro milioni 3.
Katika hoja yao ya tatu, mawakili walisema ripoti tatu za thamani ya majengo zilizoandaliwa na Wizara ya Ujenzi, muuzaji na ubalozi wa Tanzania nchini Rome hazikuandika jengo hilo lilikuwa na thamani ya chini ya euro milioni 3.
Ripoti zote ziliandika jengo hilo lilikuwa na thamani ya zaidi ya euro milioni tatu na kwamba upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha wakati huo jengo linanunuliwa lilikuwa na thamani ya kiasi gani na kwa maana hiyo jamhuri ilikuwa haifahamu thamani ya jengo hilo wakati serikali inalinunua.
“Hoja ya tano sisi tunadai kuwa upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi ambao ungeonyesha nani ni mmiliki wa akaunti mbili ambamo euro milioni 3 zilitumwa na ubalozi wa Tanzania nchini Rome.
Kwa hoja hizo tano tulizozitaja hapo juu, tunaiomba mahakama hii iwaone washtakiwa hawana hatia kwa sababu upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi ambao utaishawishi mahakama iwatie hatiani,” alidai wakili Marando.
Mahakama hiyo inatarajia kutoa hukumu yake Julai 11 kwa kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka 2007. 
Chanzo:- Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post