SIMBA WAIPIGIA MAGOTI AZAM KWA REDONDO, WATOA MILIONI 15 YAISHE WABEBE KIFAAA
Redondo |
YAMEKWISHA. Naam, sasa Simba SC na Azam FC ni amani tupu.
Azam imekubali kupokea Sh. Milioni 15 kutoka Simba SC ili kumuuza kiungo wake,
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Habari za ndani ambazo Chanzo imezipata, zimesema
kwamba hiyo inafuatia viongozi wa Simba SC kuwaangukia Azam kwa kitendo chao
cha kumsajili kiungo huyo bila kuwasiliana nao, wakati bado alikuwa ana mkataba
na Wana Lamba Lamba.
Awali, Azam walikerwa na kitendo hicho hadi wakataka kusitisha
dili la kumtoa kwa mkopo kwa Mrisho Khalfan Ngassa Simba SC. Chanzo:- http://bongostaz.blogspot.com/
Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa, baada ya kukerwa na kitendo
cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu
Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS
Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwezi uliopita.
Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea
benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa
na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga,
hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa
mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka
mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa
kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18
akipewa gari.
Inavyoonekana, Redondo aliwadanganya Simba kwamba amemaliza
mkataba na Azam, wakaingia mkenge na kumpa Sh. Milioni 30 wakimsainisha mkataba
wa miaka miwili, wakati mkataba wake na Azam unamalizika Juni mwakani.
Hili ni kosa sawa na ambalo Simba walilifanya katika usajili
mwingine wa mchezaji wa Azam, Ibrahim Rajab ‘Jeba’, miezi mitatu iliyopita
ambaye alikuwa kwa mkopo Villa Squad wao wakaenda kumsajili bila kuwasiliana na
klabu yake kujua kuhusu mkataba wake, matokeo yake baadaye mchezaji huyo
akarejea Azam.
Simba nao wana lalamiko kama hilo, dhidi ya watani wao wa
jadi, Yanga wanaowatuhumu kumsajili beki Kevin Yondan, wakati bado ana makataba
na Wekundu hao wa Msimbazi, ingawa TFF iliweka sawa kwa kusema Yondan hakuwa na
mkataba na Simba SC.
Baadaye Simba ilitoa ufafanuzi, kwamba ilimuongezea mkataba
Yondan baada ya ule wa awali kumalizika na ikawa inasubiri muda wa usajili
ufike wauwasilishe TFF. Lakini katika kesi ya awali, Simba walipoupeleka
mkataba wao mpya na Yondan, ulionyesha mchezaji huyo anatakiwa kuanza
kuutumikia mkataba huo, Desemba mwaka huu, hivyo TFF ikasema kwa wakati ambao
yuko huru, aichezee Yanga.
Sakata la Yondan litarudi Desemba, wakati ambao atatakiwa
kuanza kuutumikia mkataba wake na Simba, wakati yupo ndani ya mkataba wa miaka
miwili na Yanga.
إرسال تعليق