STARS YAWAFUATA BOTSWANA

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeondoka alfajiri ya leo kwenda Gaborone, Botswana kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kesho dhidi ya wenyeji Botswana.
Stars, inayofundishwa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali, imeondoka bila wachezaji wanne, kati ya walioitwa, wawili kipa Deo Munishi ‘Dida’ na beki Shomary Kapombe kwa sababu ni majeruhi.
Washambuliaji Mbwana Ally Samatta amezuiwa na klabu yake Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na John Bocco ‘Adebayor’ amekwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Super Sport United ya huko.
Akizungumza jana kwenye kambi ya timu hiyo, hoteli ya Somaiya eneo la Gerezani, Dar es Salaam, kocha Kim alisema anasikitika hatakuwa nao wachezaji hao kwenye safari kwa sababu hizo tofauti.
Lakini Poulsen alisema anaamini wachezaji anaokwenda nao wanaweza kumpa ushindi katika mchezo huo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa sababu amewaandaa vizuri na wameonyesha wako tayari.
Kim alisema Botswana ni timu nzuri na kwa sasa iko juu ya Tanzania kiuwezo, hivyo kama wakishinda utawasaidia kupanda kwenye viwango vya FIFA.
Kim aliwataja wachezaji watakaoondoka alfajiri ni makipa; Juma Kaseja na Mwadini Ally, mabeki; Aggrey Morris, Kelvin Yondan, Amir Maftah, Erasto Nyoni, viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Shaaban Nditi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Damayo, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa na washambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’, Simon Msuva na Said Bahanuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post