TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeondoka
alfajiri ya leo kwenda Gaborone, Botswana kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa
kimataifa kesho dhidi ya wenyeji Botswana.
Stars, inayofundishwa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen
akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali, imeondoka bila wachezaji wanne,
kati ya walioitwa, wawili kipa Deo Munishi ‘Dida’ na beki Shomary Kapombe kwa
sababu ni majeruhi.
Washambuliaji Mbwana Ally Samatta amezuiwa na klabu yake Tout
Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na John Bocco
‘Adebayor’ amekwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa
katika klabu ya Super Sport United ya huko.
Akizungumza jana kwenye kambi ya
timu hiyo, hoteli ya Somaiya eneo la Gerezani, Dar es Salaam, kocha Kim alisema
anasikitika hatakuwa nao wachezaji hao kwenye safari kwa sababu hizo tofauti.
Lakini Poulsen alisema anaamini wachezaji anaokwenda nao
wanaweza kumpa ushindi katika mchezo huo wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa sababu amewaandaa vizuri na
wameonyesha wako tayari.
Kim alisema Botswana ni timu nzuri na kwa sasa iko juu ya
Tanzania kiuwezo, hivyo kama wakishinda utawasaidia kupanda kwenye viwango vya
FIFA.
Kim aliwataja wachezaji watakaoondoka alfajiri ni makipa;
Juma Kaseja na Mwadini Ally, mabeki; Aggrey Morris, Kelvin Yondan, Amir Maftah,
Erasto Nyoni, viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Shaaban Nditi, Salum Abubakar
‘Sure Boy’, Frank Damayo, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Mrisho Ngassa na
washambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’, Simon Msuva na Said Bahanuzi.
إرسال تعليق