Wakongo nao watoweka London Olimpiki

Ujumbe wa watu wanne katika timu ya Olimpiki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoweka jijini London.
Cedric Mandembo, aliyeshiriki katika mashindano ya mchezo wa judo, na makocha wa timu za ndondi,riadha na judo hawajaonekana tokea kumalizika kwa sherehe za kufunga michezo hiyo siku ya Jumapili.
Jamhuri ya Kongo iliwakilishwa katika michezo ya London Olimpiki na wanamichezo wanne ambao hawakuweza kushinda medali yoyote. Wamamichezo hao wanatakiwa kurejea nchini mwao baadaye wiki hii.
Zaidi ya wiki moja iliyopita mabondia watano kutoka Cameroon walitoweka kutoka kijiji cha michezo hayo mashariki mwa London.
Mabondia hao waliiambia BBC kuwa wanataka kubaki nchini Uingereza ili kuendeleza taaluma zao kimichezo.
Mandembo alishiriki mashindano ya judo ya uzito wa kilo 100 jijini London lakini alitolewa katika mechi yake ya kwanza baada ya sekunde 49.
Wengine wanne maafisa waliotoweka kutoka timu hiyo ya Kongo ni kocha wa ndondi Blaise Bekwa, kocha wa riadha Guy Nkita na kocha wa judo Ibula Masengo.
Waziri wa michezo wa Kongo Baudoin amesema hana taarifa za kutosha juu ya kutoweka kwao.
"Sifahamu. Nimeondoka London asubuhi hii (jumatatu),waziri huyo alikaririwa akisema na shirika la habari la AFP.
"Jana (Jumapili) nilikuwa nao kabla ya sherehe za kufunga michezo. Walinipatia ripoti kuwa kila kitu kilikuwa kikiendelea vizuri," aliongeza.
Nchi ya Kongo imekuwa ikiathiriwa na miaka mingi ya vita ikighubikwa na umasikini licha ya maliasili yake kubwa ya madini.
Chanzo:- BBC Swahili

Post a Comment

أحدث أقدم