Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kimekutana na waandisihi wa habari makao makuu ya chama hicho
jijini Dar es Salaam jana, ambapo wajumbe wa Kamati Kuu, Profesa
Abdallah Safari na Mabere Marando, wameweka waziwazi msimamo wa chama
hicho kuhusiana na mgogoro kati ya waislamu na serikali na kukamatwa kwa
Sheikh Farid huko Zanzibar.
Wanasheria hao wa CHADEMA wamesema kuwa kitendo cha serikali kumnyima
dhamana Sheikh Ponda ni kinyume cha katiba na kwamba Chadema kama chama
kinachojiandaa kuchukua dola, hakiwezi kuvumilia kuona haki za raia
zikivunjwa.
“Tunaweza kuwa miongoni mwetu, wapo watu wanaomchukia Sheikh Ponda,
lakini hatuwezi kuficha ukweli kwamba Sheikh Ponda kama raia wa Jamhuri
ya Muungano au mkazi wa Jamhuri hii, anayo haki ya kusikilizwa na kupewa
dhamana. Makosa ambayo Sheikh Ponda ameshitakiwa yanadhaminika kwa
mujibu wa sheria, hivyo ni makosa kwa serikali kufanya hila kumnyima
dhamana kiongozi huyu wa kidini,” ameeleza Marando katika mkutano huo.
Marando alifika mbali zaidi kwa kusema tatizo lililopo sasa kati ya
serikali na waislamu, limetokana na hatua ya serikali kuwalazimisha
waislamu wote kuwa waumini wa Bakwata, chombo ambacho wengi wanakiona
kinatumika kuwakandamiza.
Naye Profesa Safari alionya matumizi ya nguvu za kijeshi yanayotumiwa
na serikali kwa kisingizio cha kulinda amani, huku akieleza kuwa
matumizi ya kijeshi siyo suluhu ya kutatua matatizo yaliopo.
Kuhusu kukamatwa kwa Sheikh Faridi na kumzuia kwa siku tatu, wanasheria hao wamesisitiza kuwa kitendo hicho hakikubaliki.
“Kitendo cha kumkamata na kumshikiria Sheikh Faridi, huku serikali na
vyombo vyake vikisema havihusiki, wakati ukweli ni kuwa alikuwa
anashikiliwa na watu wa USALAMA wa TAIFA, ni uharamia mkubwa unaopaswa
kulaaniwa na wote wanaolitakia mema taifa hili,” ameeleza Marando.
Kuhusu uvunjwaji wa makanisa, Profesa Safari amesema CHADEMA
kimelaani hatua hiyo iliyotokana na wananchi kujichukulia sheria
mkononi. Amewataka waislamu kuvuta subira.
Hata hivyo, Profesa Safari amesena matatizo yanayotokea sasa,
yameletwa na CCM kutokana na hatua yao ya kuwatumia baadhi ya waislamu
kupandikiza mbegu ya udini nchini.
إرسال تعليق