MAJANGILI wanaodaiwa kutoka nchi za Rwanda na Burundi, wameingia nchini
na kuendesha ujangili katika hifadhi ya taifa ya Ruaha na kuua tembo
zaidi ya 80 katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Wakati hali ikiwa hivyo Ruaha, watuhumiwa wanne raia wa kigeni kutoka
nchi jirani wameuawa na askari katika hifadhi ya Serengeti na kukutwa na
silaha kali za kivita.
Katika matukio ya Ruaha, majangili hao wakiwa na silaha nzito za kivita
aina ya SMG, Shot Gun, 404, 3006 na Trap Gun, wameendesha ujangili kwa
kuwatumia wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo inayozungukwa na mikoa ya
Dodoma, Mbeya na Iringa.
Akizungumza na wandishi wa habari juzi katika makao makuu ya hifadhi
hiyo, Kaimu Mhifadhi wa Idara ya Ulinzi, Edmund Murashani, alisema kuwa
ujangili umeshamiri kutokana na idadi ndogo ya askari katika hifadhi
hiyo.
Alisema kuwa majangili hayo yamekuwa yakijificha kwenye maeneo ambayo
hayafikiki kirahisi kwa magari ya doria huku hifadhi za kijamii
zikishindwa kukabiliana na ujagili huo kutokana na kuwa na silaha duni.
Murashani aliongeza kuwa wanyama wanaoongoza kuuawa ni tembo, twiga,
tandala, nyati na wengine wadogo wakiwamo swala, huku adhabu ndogo
zinazotolewa kwa wakosaji zikidaiwa kuwa ni kikwazo katika mapambano
dhidi ya ujangili.
Pamoja na kukiri kuwa silaha hizo za kivita zinatoka katika nchi hizo,
alisema wengi wa wanaokamatwa ni wananchi wa kawaida ambao wamekuwa
wagumu kutaja mtandao unaowafadhili.
Alifafanua kuwa, ucheleweshwaji wa kesi mahakamani pamoja na watuhumiwa
kuachiliwa kwa kile kinachodaiwa kukosekana kwa ushahidi wa kuwatia
hatiani ni moja ya changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo katika
kukabiliana na ujangili.
Murashani alisema kwa upande wa Dodoma majangili kutoka Rwanda huingilia
Wilaya ya Chamwino na kupolekewa na wenyeji ambao zamani walikuwa
wakitumia upinde katika kuua wanyama, lakini kwa sasa wamekuwa
wakikamatwa na silaha nzito za kivita ambazo huingizwa na majangili hao
kutoka nchi jirani.
Naye Ofisa Uhusiano mwandamizi wa Tanapa, Catherine Mbena, alisema ni
vigumu kuuhusisha mtandao wa ujangili na wafanyabiashara wakubwa kwa
vile hadi sasa hakuna kigogo yeyote aliyekamatwa.
Wanne wauawa Simiyu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Salumu Msangi alisema watuhumiwa
hao wanne ambao majina yao hayakufahamika wanakadiriwa kuwa na umri kati
ya mika 25 na 40, na kwamba walikutwa ndani ya hifadhi ya Serengeti.
Alisema kuwa Januari 22 mwaka huu, saa 11:30 jioni katika eneo la Mlima
Ngoma ndani ya hifadhi hiyo, askari wa wanyamapori wa doria walisikia
milio ya risasi mfululizo na walipofuatalitia ghafla walishambuliwa kwa
risasi mfululizo kutoka eneo hilo.
Katika majibizano hayo, majangili wanne waliuawa na bunduki aina ya SMG
isiyo na namba, risasi 367 za SMG na SAR, magazine saba za SMG, maganda
55 ya SMG, shoka moja, mapanga wawili na visu viwili vilikamatwa.
Kamanda alifafanua kuwa pia walikuta tembo mkubwa akiwa ameuawa, huku
pembe zake zikiwa zimeondolewa lakini walizipata na kuzihifadhi.
Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa mwaka 2012 jumla ya tembo
10 wameuawa ndani ya hifadhi hiyo na kundi la majangili linalosadikiwa
kutoka nchi jirani wakishirikiana na baadhi ya wazalendo.
Majangili hao wanasadikiwa kula njama na baadhi ya wananchi wa vijiji
vya Logalombogo, Mwamongo, Mwasengela, Matale, Buruti, Sakasaka katika
ukanda wa Wilaya ya Meatu inayopakana na hifadhi za pori la akiba la
Maswa na Ngorongoro.
Chanzo: Tanzania Daima
إرسال تعليق