Serikali mbalimbali duniani na mashirika ya kimataifa wanakutana leo
mjini Brussels, Ubelgiji kujadiliana namna ya kutafuta njia za kuisaidia
Mali kijeshi na kifedha pamoja na kukuza demokrasia nchini humo.
Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na
kukifadhili, kukipatia vifaa pamoja na mafunzo, kikosi cha AFISMA chenye
wanajeshi 8,000, ambacho kinatarajiwa kuchukua operesheni za kijeshi za
Mali kutoka kwa Ufaransa.
Mbali na masuala hayo, wajumbe wa mkutano huo wa kundi la kuisaidia Mali
lililoundwa mwaka uliopita, watajadiliana kuhusu mchakato wa kisiasa
nchini humo.
Afisa wa Umoja wa Ulaya amesema katika upande wa mchakato wa kisiasa
wajumbe watajadili namna ya kuisaidia Mali kufanya uchaguzi ambao rais
wa mpito wa Mali, Dioncounda Traore amesema unaweza ukafanyika mwezi
Julai mwaka huu.
Umoja wa Ulaya wafikiria msaada wa haraka
Umoja wa Ulaya unafikiria kutoa haraka kiasi cha Euro milioni 250 za
misaada ya maendeleo ambazo ilizizuia baada ya kufanyika mapinduzi mwezi
Machi, mwaka uliopita.
Maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya
Umoja huo umesema uko tayari pia kuwasaidia waangalizi wa haki za
binaadamu watakaokwenda kutafuta ushahidi kuhusu ukiukwaji wa haki za
binaadamu unaodaiwa kufanywa na waasi pamoja na wanajeshi wa Mali.
Wanadiplomasia wamesema kuwa nchi 16 wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja
na Norway zimeahidi kupeleka timu ya watu 250 kwa ajili ya kutoa mafunzo
kwa jeshi la Mali.
Mkutano huo unahudhuriwa na Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya,
Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS, Benki
ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na mashirika ya misaada.
Biden aunga mkono takwa la Ufaransa
Ama kwa upande mwingine, Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden ameunga
mkono pendekezo la Ufaransa la kutaka kukabidhi haraka operesheni za
kijeshi nchini Mali kwa vikosi vya Afrika.
Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden
Hayo ameyaeleza mjini Paris, Ufaransa baada ya kukutana na Rais Francois
Hollande, ambapo ameongeza kusema kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa
kukifanya kikosi hicho cha Afrika kama kikosi rasmi cha kulinda amani
nchini Mali, mpango ambao maafisa wa umoja huo wanasema uko katika
mchakato.
Ufaransa ina hamu ya kukabidhi operesheni za kijeshi nchini Mali kwa
wanajeshi wapatao 8,000 wa Afrika walioahidiwa kupelekwa nchini humo
baada ya kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa. Kikosi hicho cha AFISMA bado
kinapeleka wanajeshi wake taratibu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius amesema wanataka
kukabidhi operesheni hizo kwa AFISMA hasa katika miji ambayo tayari
imekombolewa. Akiwa ziarani nchini Mali, mwishoni mwa juma lililopita,
Rais Hollande aliahidi kutoiacha Mali ikiwa katika machafuko.
Post a Comment