Na Ali Adam, Mogadishu
Aman Radio itakuwa kituo cha kwanza cha redio ya wanawake wote kuleta
mawimbi ya sauti jijini Mogadishu, ikiwa na dhamira ya kuinua hali ya
wanawake wa Somalia na kuwapa mafunzo katika vyombo vya habari.
Kituo hicho, ambacho kitaanza kutoa matangazo hivi karibuni kutoka
kwenye ofisi zake katika wilaya ya Hawlwadag ya Mogadishu, itazinduliwa
na Kituo cha Habari cha Nasib na Kituo cha Mafunzo ya Vyombo vya Habari
ikiwa na ufadhili wa pesa kutoka kwa wanawake wa Somalia waliotawanyika
katika sehemu mbalimbali duniani.
Kituo hicho huwapa wanawake wasichana ambao wana shauku katika vyombo
vya habari kozi mbalimbali za uandishi wa habari, ambazo Aman Radio
itajazia kwa kuwapa wahitimu fursa ya kutendea kazi ujuzi wao katika
kituo hicho.
Sabahi ilimhoji Mkurugenzi Msaidizi wa Aman Radio Farhia Farah Roble kujua zaidi kuhusu mipango ya kituo hicho kipya.
Sabahi: Kwa nini kuanzisha kituo ambacho kinaajiri wanawake tu?
Farhia Farah Roble: Kinakusudiwa kuwawezesha wanawake, hususani katika vyombo vya habari. Kama unavyojua, Mogadishu ina vituo vingi vya redio, lakini hakuna inayosimamiwa na mwanamke.
Sabahi: Kwa nini mmechagua kituo cha redio kuwawezesha wanawake na sio shule au kitu kingine?
Roble: Tumechagua kuanza na redio kwa sababu kusoma hakujaenea
nchini Somalia [kwa sasa], na tulitaka [kuchagua chombo] ambacho
kitatusaidia na kusambaza ujumbe wetu wa uwezeshaji kwa wanawake wote wa
Somalia. Hii ndiyo maana tulitaka kuanzisha chombo cha habari
kinachomilikiwa na kuendeshwa na wanawake.
Sabahi: Je, mmekabiliwa na vikwazo vyovyote?
Roble: Wakati wowote unapoanza kitu kipya lazima utarajie
changamoto, lakini hadi sasa hatujakabiliwa na vikwazo vyovyote. Ukweli
ni kwamba, kuna watu wanaosema kwamba kituo cha redio kinachoendeshwa na
wanawake hakitakuwa na thamani yoyote [kwa jamii], lakini maoni kama
hayo hayana maana.
Sabahi: Wazo la Radio Aman lilijitokeza lini?
Roble: Wazo lilikuja miaka sita iliyopita, wakati Kituo cha
Mafunzo ya Habari kwa Wanawake cha Nasib kilipoanza kuchapisha magazeti
ambayo yanatoa habari zinazohusu wanawake. Kituo hicho pia kinatoa
mafunzo ya uandishi wa habari kwa wasichana ambayo yanahusisha kozi za
maarifa ya ufundi katika uhariri na upigaji picha za video. Kila baada
ya miezi sita tunazalisha wahitimu 60. Sasa inawezekana kwetu kuanzisha
kituo cha redio pamoja na wahitimu hao wote.
Sabahi: Je ni malengo yapi mnayotaka kuyatimiza?
Roble: Tunataka wanawake wa Somalia kujitegemea na kuweza
kufanya kazi zinazofanywa na wanaume, ama kazi za uga wa ufundi wa
uandaaji wa vipindi, kuripoti au kuhariri.
Sabahi: Je, ni kwa jinsi gani vipindi vyako vya redio vitasaidia kuendeleza lengo hilo?
Roble: Tutaandaa vipindi ambavyo vinalenga katika elimu ya
wasichana wadogo na [kusheherekea] michango chanya ambayo wanawake wa
Somalia wameifanya katika jamii wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Tutawaalika wanazuoni wa Somalia kutusaidia kuelezea wajibu chanya ambao
wanawake wameshafanya na kujadili changamoto zinazowakabili sasa.
Sabahi: Tueleze kuhusu wafanyakazi wako
Roble: Kwa sasa tuna wafanyakazi 25. Hawa ni pamoja na mafundi
mitambo wa redio, maripota na wapiga picha, wote ambao wamemaliza
programu zetu za mafunzo.
Sabahi: Mnaonekana kuwa na timu changa sana. Je, watakuwa wakilipwa?
Roble: Wanawake wanaofanya kazi katika Kituo cha Aman Radio ni
wenye umri wa miaka kati ya 17 na 20. Baadhi yao wanapokea mshahara
wakati wengine bado wanakamilisha kozi zao.
Sabahi: Je, kituo chako bado kitaendelea na programu ya mafunzo?
Roble: Kituo cha Nasib kitaendelea na kazi yake ya mafunzo na
kutoa fursa kwa wanawake. Kituo kilianzishwa kama sehemu ya lengo hilo,
hivyo mafunzo yataendelea.
Post a Comment