MrJazsohanisharma

Redio inayoendeshwa na wanawake kufunguliwa nchini Somalia

Mtangazaji wa Aman Radio Ubah Said akifanya mazoezi ya kusoma kwenye redio kabla ya kituo kuanza kutoa matangazo. [Ali Adam/Sabahi]

Na Ali Adam, Mogadishu

Aman Radio itakuwa kituo cha kwanza cha redio ya wanawake wote kuleta mawimbi ya sauti jijini Mogadishu, ikiwa na dhamira ya kuinua hali ya wanawake wa Somalia na kuwapa mafunzo katika vyombo vya habari.
Kituo hicho, ambacho kitaanza kutoa matangazo hivi karibuni kutoka kwenye ofisi zake katika wilaya ya Hawlwadag ya Mogadishu, itazinduliwa na Kituo cha Habari cha Nasib na Kituo cha Mafunzo ya Vyombo vya Habari ikiwa na ufadhili wa pesa kutoka kwa wanawake wa Somalia waliotawanyika katika sehemu mbalimbali duniani.
Kituo hicho huwapa wanawake wasichana ambao wana shauku katika vyombo vya habari kozi mbalimbali za uandishi wa habari, ambazo Aman Radio itajazia kwa kuwapa wahitimu fursa ya kutendea kazi ujuzi wao katika kituo hicho.
Sabahi ilimhoji Mkurugenzi Msaidizi wa Aman Radio Farhia Farah Roble kujua zaidi kuhusu mipango ya kituo hicho kipya.
Sabahi: Kwa nini kuanzisha kituo ambacho kinaajiri wanawake tu?
Farhia Farah Roble: Kinakusudiwa kuwawezesha wanawake, hususani katika vyombo vya habari. Kama unavyojua, Mogadishu ina vituo vingi vya redio, lakini hakuna inayosimamiwa na mwanamke.
Sabahi: Kwa nini mmechagua kituo cha redio kuwawezesha wanawake na sio shule au kitu kingine?
Roble: Tumechagua kuanza na redio kwa sababu kusoma hakujaenea nchini Somalia [kwa sasa], na tulitaka [kuchagua chombo] ambacho kitatusaidia na kusambaza ujumbe wetu wa uwezeshaji kwa wanawake wote wa Somalia. Hii ndiyo maana tulitaka kuanzisha chombo cha habari kinachomilikiwa na kuendeshwa na wanawake.
Sabahi: Je, mmekabiliwa na vikwazo vyovyote?
Roble: Wakati wowote unapoanza kitu kipya lazima utarajie changamoto, lakini hadi sasa hatujakabiliwa na vikwazo vyovyote. Ukweli ni kwamba, kuna watu wanaosema kwamba kituo cha redio kinachoendeshwa na wanawake hakitakuwa na thamani yoyote [kwa jamii], lakini maoni kama hayo hayana maana.
Sabahi: Wazo la Radio Aman lilijitokeza lini?
Roble: Wazo lilikuja miaka sita iliyopita, wakati Kituo cha Mafunzo ya Habari kwa Wanawake cha Nasib kilipoanza kuchapisha magazeti ambayo yanatoa habari zinazohusu wanawake. Kituo hicho pia kinatoa mafunzo ya uandishi wa habari kwa wasichana ambayo yanahusisha kozi za maarifa ya ufundi katika uhariri na upigaji picha za video. Kila baada ya miezi sita tunazalisha wahitimu 60. Sasa inawezekana kwetu kuanzisha kituo cha redio pamoja na wahitimu hao wote.
Sabahi: Je ni malengo yapi mnayotaka kuyatimiza?
Roble: Tunataka wanawake wa Somalia kujitegemea na kuweza kufanya kazi zinazofanywa na wanaume, ama kazi za uga wa ufundi wa uandaaji wa vipindi, kuripoti au kuhariri.
Sabahi: Je, ni kwa jinsi gani vipindi vyako vya redio vitasaidia kuendeleza lengo hilo?
Roble: Tutaandaa vipindi ambavyo vinalenga katika elimu ya wasichana wadogo na [kusheherekea] michango chanya ambayo wanawake wa Somalia wameifanya katika jamii wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tutawaalika wanazuoni wa Somalia kutusaidia kuelezea wajibu chanya ambao wanawake wameshafanya na kujadili changamoto zinazowakabili sasa.
Sabahi: Tueleze kuhusu wafanyakazi wako
Roble: Kwa sasa tuna wafanyakazi 25. Hawa ni pamoja na mafundi mitambo wa redio, maripota na wapiga picha, wote ambao wamemaliza programu zetu za mafunzo.
Sabahi: Mnaonekana kuwa na timu changa sana. Je, watakuwa wakilipwa?
Roble: Wanawake wanaofanya kazi katika Kituo cha Aman Radio ni wenye umri wa miaka kati ya 17 na 20. Baadhi yao wanapokea mshahara wakati wengine bado wanakamilisha kozi zao.
Sabahi: Je, kituo chako bado kitaendelea na programu ya mafunzo?
Roble: Kituo cha Nasib kitaendelea na kazi yake ya mafunzo na kutoa fursa kwa wanawake. Kituo kilianzishwa kama sehemu ya lengo hilo, hivyo mafunzo yataendelea.

Post a Comment

أحدث أقدم