Askari wa Polisi wakituliza Ghasia jijini Arusha.(Picha na Maktaba).
Na Anna Nkinda – Maelezo, Mbeya
Watanzania wametakiwa kupiga magoti na kuomba kila mtu kwa imani yake ili Mwenyezi Mungu aweze kuwalaani watu ambao wanatishia kuvuruga amani ya nchi na kusababisha chuki katika jamii.
Wito huo umetolewa leo na Chifu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Rocket Mwashinga wakati akiongea na wakazi wa Ushirika wilayani Rungwe kwenye mazishi ya George Mwaikela aliyefariki Dunia jijini Dar es Salaam kwa ajali ya gari.
Chifu Mwashinga lmeema kuwa hali iliyopo nchini hivi sasa si nzuri kwani kuna baadhi ya makundi ya watu wanataka kuwalambisha watanzania sumu mbaya ya chuki ya udini na kuwaomba wasiilambe sumu hiyo bali kila mmoja kwa imani yake apige magoti na kumuomba Mwenyezi Mungu ili amani iliyopo iendelee kuwepo.
Amesema kuwa marehemu George alikuwa ni kijana mdogo wa kwanza na wa ajabu aliyeweza kuwafuata machifu na kuwapa ushauri mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuata mila nzuri na kuachana na mila ambazo zimepitwa na wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abas Kandoro amesema kuwa binadamu anaweza kupata madhara kwa kutokumtii Mwenyezi Mungu na katika kitu kibaya ambacho kinaanza kutokea katika jamii ya watanzania ni pamoja na kubaguana katika misingi ya dini hali ambayo itasababisha watu kuuana.
Mh. Kandoro amesema, “Tumekusanyika hapa kuja kumzika ndugu yetu si kwa itikadi ya dini bali ni binadamu mwenzetu, tulikuwa tunaishi naye kwa amani na upendo na sisi sote mbele ya Mwenyezi Mungu ni kitu kimoja na matendo yetu katika dunia ndiyo yatakayotufanya tuuone ufalme wa Mungu.
Naye Baba Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu Ruanda Padre Peter Malya amewataka watanzania kuishi maisha yanayoendana na ubinadamu na ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na kuachana na matendo ya kinyama.
Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali walihudhulia mazishi hayo akiwemo Mke wa Rais Mh. Mama Salma Kikwete na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mh. Adam Malima.
إرسال تعليق