YANGA YAICHAPA 1-0 3PILLARS

Kikosi cha Young Africans kilichoanza leo dhidi ya 3 Pillars

Young Africans imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya 3 Pillars FC kutoka Lagos Nigeria katika mchezo wa kirafiki uliofanyika leo jioni katika dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara Young Africans waliingia uwanjani kwa lengo la kusaka ushindi na kuendeleza rekodi ya ushindi katika michezo ya kirafiki ya kujipima nguvu inayocheza kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom 2013/2014.

Ikiwa tumia washambuliaji wake wapya Hussein Javu na Mrisho Ngassa waliojiunga na kikosi msimu huu, Yanga ilikosa nafasi za wazi za kufungua kupitia kwa washambuliaji hao ambao hawakuonekana kuwa makini makini katika umaliziaji wa mipira iliyokuwa ikiwafikia.

David Luhende alikosa bao dakika ya 34 kufuatia mpira alioupiga kuokelewa na mlinda mlango wa 3Pillars FC na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda, huku awali Said Bahanuzi akikosa nafasi pia kama hiyo dakika ya 17 ya mchezo.

Hussein Javu aliipatia Young Africans bao kwanza dakika ya 40 ya mchezo kwa ustadi akiitumia vizuri nafasi hiyo aliyopewa na kuingo Athuman Idd 'Chuji' aliyewazidi ujanja walinzi wa 3Pillars FC na kumpasia Javu aliyeukwamisha mpira wavuni na kuhesabu bao kwa watoto wa Jangwani.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Young Africans -0 3Pillars FC.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ambapo Yanga iliwaingiza Didier Kavumbagu, Kelvin Yondani, Oscar Joshua, na Salum Telela kuchukua nafasi za Nadir Haroub, Jerson Tegete, Juma Abdul na Said Bahanuzi mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mchezo.

David Luhende ambaye leo alikuwa mwiba kwa timu ya 3Pillars FC nusura aipatie Yanga bao la pili lakini mpira alioupiga ulikokolewa na walinzi wa timu hiyo ya Nigeria na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Yanga iliendelea kulishambulia lango la 3Pillars dakika zote za mchezo lakini kutokua makini kwa mshambuliaji Didier Kavumbagu na Hussein Javu kuliendelea kuufanya ubao wa mabao uendelee kusomeka 1-0.

Mpaka dakika 90 za mwamuzi Oden Mbaga zinamalizika, Young Africans 1-0 3Pillars FC .

Kesho kikosi cha Yanga hakitakua na mazoezi na wachezaji wote watakua na mapumziko kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Eid na waterejea tena mazoezini siku ya jumamosi asubuhi katika uwanja wa Loyola kuendelea kujifua na maandalizi ya Ligi Kuu.

Young Africans: 1.Ally Mustapha 'Barthez', 2.Juma Abdul/Salum Telela, 3.David Luhende, 4.Nadir Haroub 'Cannavaro'/Kelvin Yondani, 5.Rajab Zahir, 6.Athuman Idd 'Chuji/Issa Ngao, 7.Said Bahanuzi/Abdallah Mguhi 'Messi'/Shaban Kondo, 8.Haruna Niyonzima/Bakari Masoud, 9.Jerson Tegete/Didier kavumbagu, 10.Hussein Javu, 11.Mrisho Ngassa

Post a Comment

Previous Post Next Post